Wanafunzi eneo bunge la Kilifi kusini wataendelea kupata ufadhili wa masomo ya sekondari na chuo kikuu maarufu National Scholarship Fund baada ya mpango huo kusitishwa kwa muda kutokana na mapendekezo ya kuondolewa kwa hazina ya ustawi wa maeneo bunge CDF.
Mpango huo wa hazina ya kitaifa ya ufadhili wa masomo unaofanyika katika eneo bunge la Kilifi Kusini ulioanzishwa mnamo mwaka 2018, uliwaacha wanafunzi wengi wakiwa na wasi wasi.
kwa sasa ni dhahiri kwamba licha ya kusitishwa kwa muda, mpango huo utaendelea kufuatia bunge la kitaifa kuunga mkono kuendelea kuwapo kwa hazina ya ustawi wa maeneo bunge NGCDF.
Mbunge wa Kilifi Kusini Ken Chonga, amepongeza hatua ya rais William Ruto ya kuhakikisha kuwa NGCDF inaendelea kuwapo ili wanafunzi waendelee kusaidika katika ufadhili wa masomo.
Chonga ameongeza kuwa hadi kufikia sasa wanafunzi zaidi ya 370 wamefanikiwa kujiunga na vyuo vikuu humu nchini kupitia mpango huo wa ufadhili.
Aidha ameeleza kuwa mpango huo unaendelea kuwafaidi wanafunzi wengi zaidi huku akisema hakuna mwanafunzi kutoka eneo bunge hilo atakaye salia nyumbani kwa ukosefu wa karo.
BY ERICKSON KADZEHA