Wawakilishi wadi katika kaunti ya Kilifi wanaitaka serikali ya kitaifa
kutenga mgao wa fedha wa maendeleo ya wadi ili kuhakikisha kuwa
wanafunzi wa Junior Secondary wananufaika na fedha za ufadhili wa elimu
maarufu basari kutoka kwa serikali kitaifa.
Kulingana na diwani wa Mnarani Juma Chengo, serikali ya kitaifa inafaa
kubuni mfuko wa maendeleo ya wadi ambao utakua chini ya waakilishi wadi,
akisistiza kuwa mzigo wa basari kwa wanafunzi umeongezeka kutokana na
wazazi kuwatafuta ili kuwasaidia na watoto wao wanaojiunga na Junior
Secondary kufuatia gharama za juu zinazoambatana na mfumo huo mpya wa
elimu.
Anasema kwa sasa asilimia 35 ya mgao wa fedha unaotoka katika serikali
ya kaunti hautoshi kutokana na mzigo wa CBC ambao umeongezwa katika
mikono ya viongozi hao wa kaunti.
Haya yanajiri baada ya spika wa bunge la Kilifi Teddy Mwambire kueleza
kuwa tayari majadiliano yanaendelea kati ya mabunge ya kaunti za Kenya
ili kuhakikisha wakati mabadiliko ya kikatiba kuhusu mgao wa fedha wa
NG-CDF yanafanyika yaambatane na mabadiliko kuhusu fedha za maendeleo ya
wadi.
BY ERICKSON KADZEHA.