Rais William Ruto ameahidi kutimiza ahadi zake zote alizoahidi Wakenya wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.
Akihutubia wakenya katika Ikulu ya rais jijini Nairobi wakati wa kusainiwa kwa Mikataba ya Utendaji kazi na mawaziri, Rais Ruto, amewataka wakenya kuwa na subra kwani ameweka mikakati thabiti ya kutimiza ahadi zake kabla ya awamu ya kwanza kukamilika.
Wakati uo huo rais ametoa onyo kwa Mawaziri na Wakuu wa mashirika mbalimbali ya kiserikali kuwa watachukuliwa hatua iwapo watashindwa kuwajibika katika majukumu yao serikalini.
Kiongozi huyo wa nchi aidha amewataka mawaziri wake kutia bidii katika kazi zao ili kufanikisha ajenda zake kuu za kubadilisha maisha ya Wakenya akiongeza kuwa serikali yake haitamsaza Waziri atakayezembea kazini.
“Lazima tufanye kazi kwa bidii na bora zaidi ili kutimiza ahadi zetu. Tunayo nafasi ya kubadilisha nchi yetu,” alisema Rais.
Ruto aidha amewahakishia Wakenya kuwa serikali yake haitakubali kiongozi yeyote au mfanyakazi ambaye ataendeleza ufisadi kuhudumu ndani ya serikali yake huku akiwataka mawaziri wake kuwafuta kazi watakaopatikana.
“Hatutasubiri hadi pesa zitakapopotea. Tutakabiliana nayo pindi tutakapoona dalili zake.”
Alisisitiza kuwa hakutakuwa na pesa za kuiba bali za kutekeleza programu za Serikali.
Rais alikuwa akizungumza wakati wa kusainiwa kwa Mikataba ya Utendakazi wa Mawaziri ya mwaka wa kifedha wa Serikali wa 2023/2024 katika Ikulu ya Nairobi.
Rais aidha ameonyesha kughadhabishwa na hatua ya kuwa baadhi ya wakuu serikali wakiwemo Mawaziri, Makatibu pamoja Wakuu katika Idara mbali mbali hawana ufahamu kuhusu majumu yao.
Naibu Rais Rigathi Gachagua, Mkuu wa Baraza la Mawaziri Musalia Mudavadi, Mawaziri, Magavana, Mshirikishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa Stephen Jackson, miongoni mwa viongozi wengine, walihudhuria.
BY EDITORIAL DESK