Wizara ya afya kaunti ya Kwale imethibitisha mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu, katika kaunti hiyo huku kesi 5 zikiripotiwa mwezi huu katika eneo la Darad huko Msambweni.
Akithibitisha mkurupuko wa ugonjwa huo Waziri wa Afya Kaunti ya Kwale Francis Gwama amesema kati ya mwezi Mei na Juni kesi 14 ziliripotiwa katika eneo la Tiwi na Gombato huku Dzivani na Lutsangani pia kukiripotiwa kesi 14.
Katika kipindi cha muda huo aidha iliripotiwa kuwa watu wawili eneo la Tiwi na mtoto mmoja wa miaka 8 eneo la Lutsangani walipoteza maisha.
Gwama ameeleza kwamba tayari Wizara hiyo imeanzisha mpango wa kutibu maji kwenye mabwawa huku akiwataka wakaazi kuzingatia kanuni za usafi ili kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo unaotokana na mazingira machafu.
“Kinga ni kuwa na behavior change, tutibu maji tunayokunywa na tutumie vyoo ipasavyo tutaweza kudhibiti hali hii. Kwa sababu dalili ya kwanza ni kutapika na kuhara yaani effortless diarrhea na hali inakuwa mbaya zaidi kwa watoto chini ya miaka 5,” alisema Gwama
Wakati uohuo amewataka wafanyabiashara wa vyakula kuzingatia kanuni za usafi kutoka kwa wizara ya afya ama wafunge biashara hizo.
“kama wewe unahatarisha maisha ya umma, kwa kutozingatia viwango vya usafi biashara hiyo tutaifunga. Mambo ya chakula lazima usafi uwe hali ya juu, nje kuwa na maji na sabuni ili kusiwe na maambukizi.”
NA BINTIKHAMIS MOHAMMED