HabariKimataifaLifestyle

Uamuzi wa Mahakama ya Upeo kuruhusu Jumuiya ya LGBTQ wazua Tumbojoto

Wabunge wa Mombasa wamepewa makataa ya siku 7 kuwasilisha hoja bungeni kupinga hatua ya Mahakama ya juu kuruhusu LGBTQ kuwa na mashirika.

Vuguvugu la kupinga mapenzi ya jinsia moja mjini Mombasa limepinga uamuzi wa Mahakama ya Juu uliothibitisha haki ya washirika hao wa mapenzi ya jinsi moja kujumuika nchini.

Vuguvugu hilo limesema kuwa halikubaliani na uamuzi wa mahakama hiyo na wamesema wabunge wanapaswa kupinga hatua ya Mahakama ya juu na kutoruhusu usajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayounga mkono LGBTQ.

“Kile Mahakama hiyo ya Upeo imeamua, tunakipinga kwa kauli moja na kukemea vikali. Tunatoa wito vyama vya LGBTQ visisajiliwe na wabunge wapinge kwa kauli moja. Tunamtaka msajili wa mashirika ya kijamii apuuzilie mbali uamuzi huo na asiruhusu usajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayounga mkono hayo,” walisema.

Nao viongozi wa dini mjini Mombasa siku ya Jumatano waliandamana wakipinga uamuzi huo wa mahakama ya upeo wakiutaja Kwenda kinyume na dini, maadili na tamaduni za Kiafrika.

Wakiongozwa na Sheikh Mohammed Khalifa, viongozi hao waliitaka Idara hiyo ya mahakama kuendeleza majukumu yao kulingana na misingi na katiba ya taifa huku wakiitaka mahakama hiyo kubadili uamuzi huo.

“Tunawaambia waliotoa uamuzi huo hili jambo hatutalikubali, sisi hatutambui, hatukubali na hatutashirikiana na wao kabisa. Tutaendelea kupinga vitendo vyote vya LGBTQ, tumesiimama kidete kulinda maadili ya watoto wetu, maadili yetu na kuheshimu vitabu vya Mwenyezi Mungu, hili jambo la kuharibu maadili ya taifa la Kenya na heshima ya wananchi wa Wakenya,” alisema Sheikh Khalifa.

Wakati huo huo Kamati ya kusimamia utamaduni na michezo ilipinga vikali uamuzi huo wa mahakama ya juu kuruhusu watu wanaopigia debe mapenzi ya jinsia moja kuwa na vuguvugu lao hapa nchini.

Dkt. Kasisi Jackson Kosgei ambaye ni mbunge maalum na mwanakamati wa kamati hiyo na aliutaja uamuzi huo kuwa ni kinyume cha katiba na dini kwa ujumla huku akisema utaharibu vizazi vijavyo.

“Kamati ya tamaduni na michezo iliyotwikwa jukumu la kufuatilia masuala yanayohusu tamaduni, inakemea vikali uamuzi wa Mahakama ya Juu kuruhusu kusajiliwa kwa mashirika ya LGBTQ. Hii ni kuharibu tamaduni zetu nzuri za kitaifa na katiba inatambua ukubwa na utukufu wa Mwenyezi Mungu na heshima,” alisema Kasisi Kosgei.

Itakumbukwa kuwa mnamo siku ya Jumanne Septemba 12 Mahakama ya Juu nchini Kenya ilitupilia mbali rufaa ya kesi iliyowasilishwa kupinga washirika wa mapenzi ya jinsia moja kuunda muungano na mashirika yao.

Mahakama hiyo ya kilele iliruhusu kusajiliwa kwa mashirika ya LGBTQ kuwa na uwakilishi wa kutetea maslahi na haki zao.

BY EDITORIAL DESK