HabariNews

Mchungaji Ezekiel Odero hana hatia! Mahakama yamwondolea kesi

Hatimaye Mashtaka yaliyokuwa yakimkabilia mchungaji Ezekiel Odero wa kanisa la New Life yamefutiliwa mbali.

Mahakama ya Shanzu mjini Mombasa mnamo Jumanne Oktoba 31, ilimwondolea mashtaka Pasta Ezekiel yaliyokuwa yakimhusisha na mauaji ya halaiki ya Shakahola.

Hakimu Mkuu Mwandamizi katika mahakama ya Shanzu Joe Omido aliamuru kesi hiyo ifungwe kufuatia agizo la Kiongozi wa mashtaka ya Umma, DPP kutaka kesi hiyo ifungwe baada ya uchunguzi kukamilika.

Jaji Omido alisema hakuwa na chaguo jingine ila kuisitisha kesi hiyo mara moja na kumwondolea mashtaka Ezekiel baada ya kutathmini kwa kina maombi ya mshtakiwa na utetezi wa kesi hiyo.

Wakili wa pasta Ezekiel, Wyclif Ombeta, alikuwa ameutaja mchakato wa kesi hiyo kuchukua muda mrefu pasi kuamuliwa wala kuendelezwa kwa kesi na kuitaka mahakama iondoe kesi hiyo.

Kwa upande wake DPP alisema kufuatia uchunguzi walioufanya wa kina waliafikiana hakuna ukweli wowote kuhusiana na madai hayo na hivyo kesi hiyo ikawekwa kalamu mapema leo.

Mchungaji huyo alikuwa akituhumiwa kwa madai ya mauaji, utekaji nyara, kusaidia kujiua, uhalifu dhidi ya ubinadamu,ukatili wa watoto ulaghai na utalatishaji wa fedha.

Haya yanajiri majuma kadhaa baada ya Ezekiel kufika mbele ya kamati ya bunge la Seneti inayochunguza mauaji ya Shakahola kujibu maswali kuhusiana na madai ya kuhusishwa kwake na kesi hiyo.

Baada ya kueleza mengi bungeni kuhusu Kanisa lake na hata kukana madai mbalimbali alioyohusishwa nayo, Odero aliwaalika wanakamati wa kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa kaunti ya Tanariver Danson Mungatana.

Kamati hiyo ilibaini kuwa hakukuwa na makaburi ya halaiki wala mochari katika kanisa lake Ezekiel eneo la Mavueni na kuahidi kutoa ripoti yake kamilifu.

BY MJOMBA RASHID