HabariMazingiraMombasa

Subira yavuta heri! Serikali yaidhinisha malipo ya ziada kwa Wafanyakazi wa KPA

Hatimaye serikali imeidhinisha malipo ya ziada ya mwezi mmoja kwa wafanyakazi wote wa halmashauri ya bandari nchini KPA baada ya miaka mitatu ya kusubiri.

Akizungumza hapa Mombasa waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen amesema hatua hiyo inalenga kuwapa motisha wafanyakazi hao ili kufanikisha utendakazi bora katika bandari.

Murkomen alieleza baadhi ya mikakati wanayopania kutekeleza ili kuhakikisha shughuli za bandari humu nchini zinaendeshwa vilivyo ikiwemo upanuzi wa bandari kwa kukamilisha mradi wa ujenzi wa Dongokundu.

“Utendakazi bora ulioshuhudiwa katika bandari haikuweza kufikiwa bila mchango wa wafanyakazi wake, matokeo ya ukaguzi wa utendakazi katika mwaka 2020-2021 halmashauri imenakili ubora wa matokeo ya uendeshwaji wa shughuli zake. Kufuatia suala hilo licha ya kucheleweshwa,ninafuraha kutangaza kuwa serikali imeidhinisha malipo ya ziada ya mwezi mmoja kwa kila mfanyakazi wa bandari nchini,” alisema Murkomen.

Waziri Murkomen amesisitiza haja ya serikali kupewa uhuru wa kuamua masuala ya utekelezwaji wa mipango ya serikali nchini kama njia mojawapo ya kufanikisha miradi ya maendeleo kwa muda ufaao.

Ametaja ya changamoto hiyo kama kikwazo katika kukamilisha miradi ya maendeleo nchini huku akiitaka serikali kubadili baadhi ya sera na sheria zinazohusisha masuala hayo.

“Najua tunajitambua taifa hili kuwa la kidemokrasia lakini tusitumie mfumo wetu wa serikali kuchelewesha ukuaji wa taifa. Kuna vitu tunaiga kutoka kwa mataifa jirani na tunahitaji kuiga kutoka taifa la Rwanda kutokana na jinsi wanavyoendesha taifa lao kwa sababu mfumo wao huruhusu uongozi kuu kufanya maamuzi muhimu na kuwawezesha kutekeleza miradi yao ya maendeleo haraka. Kama taifa tunapaswa kuangalia sheria zinazozunguka masuala ya maamuzi,” alisisitiza Murkomen.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Nahodha William Ruto na mwenzake Benjamin Tayari ambaye ni mwenyekiti wa Bodi ya Wasimamizi wa Bandari wamepongeza wafanyakazi wa bandari kwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo huku akiwahimiza kutia fora zaidi ili kuenua taifa kiuchumi.

“Nataka kuwashukuru wafanyakazi wenzangu ni kwa sababu yao tumeweza kufikia malengo yetu,” alisema Capt. Ruto.

“Wanafanya kazi saa 24 kuhakikisha kwamba bandari inasonga mbele, nataka kukuhakikishia waziri kwamba viwango tulivyomkambidhi mkurugenzi kufikia sasa tunaona anafanya vizuri,tumeamua kwamba tutafanya kazi na tutapeleka pesa kwa serikali kuu ili ijenge taifa letu la Kenya.” Aliongeza Tayari.

BY NEWSDESK