Serikali imebaini kwamba jumla ya watu 174 walipoteza maisha yao kufuatia mvua kali ya El Nino iliyoshuhudiwa katika maeneo tofauti nchini mwishoni mwa mwaka jana.
Haya ni kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa na kituo cha kitaifa cha maagizo ya dharura na kukabiliana na mafuriko ya El Nino nchini. Kati yao, 133 walikuwa watu wazima huku 41 wakitajwa kuwa watoto wwenye umri mdogo.
Takriban wanyama 6700 walifariki wakati wa msimu huu wa mvua huku mazao yenye thamani ya shilingi bilioni 16 yakiharibiwa.
Fauka ya hayo, Idara ya Hali ya Hewa nchini imewashauri Wakenya kutarajia hali ya jua na ukame kote nchini hadi angalau mwishoni mwa mwezi Januari 2024.
Hata hivyo, mikoa mahususi ikiwa ni pamoja na bonde la Ufa maeneo ya Ziwa Victoria na ukanda wa Pwani yanatarajiwa kupata mvua za hapa na pale.