Kampuni ya ndege ya Fly Dubai imezindua safari za moja kwa moja kutoka Dubai hadi Mombasa Januari 17, 2024.
Akizungumza na wanahabari katika hafla ya kuzindua rasmi safari hizo hapa Mombasa waziri wa Barabara na uchukuzi Kipchumba Murkomen alipongeza hatua hiyo akisema itafungua milango kwa watalii zaidi kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni kuzuru taifa hili.
Murkomen alisema serikali imeweka mikakati mwafaka kuhakikisha kuwa wadau mbalimbali wananufaika kikamilifu na sekta ya utalii ikizingatiwa kuwa ni mojawapo ya vitega uchumi vikuu vya taifa.
“Wataleta bidhaa mpya nchini kutokana na ushirikiano mwema baina yao na mataifa ya mashariki mwa ulaya.ni muhimu kuwezesha wakenya wanaosafiri kuelekea Dubai na watalii wanaozuru kenya kupitia Dubai.Tunafahamu kumekuwa na changamoto za stakabadhi za usafiri na sisi kama serikali tunajitahidi kuhakikisha kuwa yanatatuliwa ili kuhakikisha tunaongeza idadi ya watalii wanaozuru nchini.”Alisema Murkomen.
Naye Gavana wa kaunti ya Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir alisema kuwa ufanikishwaji wa angahuru nchini kutaimarisha utalii wa Pwani na taifa kwa jumla kwa kuongeza idadi ya watalii wanaozuru eneo hilo.
“Suala hii halitafaidi kaunti ya Mombasa pekee bali ukanda mzima wa Pwani na ujio wa Fly Dubai utafanya Mombasa kufikiwa na watu kutoka maeneo mengi ulimwenguni.Hivi karibuni tutashudiwa ndege nyingi zitakazokuwa zinasafirisha watalii kutoka angatua ya Mombasa hadi maeneo mengine ya hapa Pwani.”Alisema Gavana Nassir.
Kwa upande wake naibu afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya Fly Dubai Sudhir Sreedharan alieleza kuwa kupitia safari hizo zitachangia ukuaji wa sekta ya utalii na uchumi wa taifa kwa jumla akiahidi kushirikiana na wadau husika ili kufanikisha huduma bora kwa wateja wao.
“Tunatarajia kuhudumia soko na kusaidia mtiririko wa biashara baina ya kenya na mataifa ya uarabuni .Tunaimani kuwa wageni kutoka mataifa ya uarabuni na ulimwenguni watafurahia vivutio vya Mombasa.Safari hizo zitasaidia kuimarisha hadhi ya mombasa kama kitovu cha biashara na utalii.
Kampuni ya ndege ya Fly Dubai ni kampuni ya kwanza kutoka Uarabuni kuruhusiwa kuendeleza safari za moja kwa moja mara nne kwa wiki na tunapania kuongeza idadi ya safari hizo katika siku za usoni.” Alisema sudhir.