Wandani wa rais huko eneo la Bonde la Ufa wakizidi kuikosoa na kuisuta Idara ya Mahakama kwa kile wanachodai kuwa inahujumu miradi muhimu ya serikali.
Wakizungumza Jumapili kwenye hafla ya mchango katika shule ya upili ya Metkei eneobunge la Keiyo Kusini kaunti ya Elgeyo Marakwet, Viongozi hao Farouk Kibet ambaye ni msaidizi wa rais, Waziri wa vyama vya Ushirika na biashara ndogo Simon Chelugui na Seneta wa Nandi Samson Cherargei walisema kuwa hawana imani na idara hiyo kwani imesitisha zaidi ya miradi Mitatu ya serikali.
Viongozi hao walibaini kuwa watafuatilia kwa karibu uchaguzi wa chama cha Mawakiliu nchini LSK, na kuhakikisha kuwa watakaochaguliwa watakuwa wakiunga mkono ajenda za rais Ruto na serikali yake.
“Hatuwezi kuendelea hivi, Kila kitu mahakama inasimamisha, kuna uchaguzi wa LSK ambayo itafanywa, tutasafisha hiyo nyumba ndio tuhakikishe wale wanachaguliwa officials wanaunga ajenda za rais.” Alisema Kibet.
Seneta wa Nandi Samson Cherargei aidha aliongeza kuwa idara ya mahakama Inashirikiana na viongozi wengine kumpiga vita Rais William Ruto ambaye anasema Yuko na mipango ya kuimarisha sekta muhimu zitakazowafaidi wananchi.
“Kortini inasimama mbele ya manifesto ya Wakenya. President ama Kiongozi yoyote anachaguliwa kwa sababu ya manifesto yake kwa watu. Na nina uhakika hata mtu akienda kortini kusimamisha hii mbolea inagawanywa mahakama itazuia,” alisema.
BY CYNTHIA OCHIENG