HabariLifestyleNews

Mvua Kubwa Kuongezeka Ijumaa hadi Jumapili, Idara ya Hali ya Anga Yatahadharisha

Idara ya hali ya anga nchini, MET imetoa tahadhari ya mvua kubwa zitakazoanza leo Ijumaa na kuendelea kwa siku mbili zaidi.

Katika taarifa yake Mkurugenzi wa Idara hiyo Dkt. David Gikungu amesema ongezeko la mvua kubwa zaidi ambayo huenda ikaandamana na mafuriko itadhuudiwa jijini Nairobi, eneo la Pwani, Bonde la Ufa, eneo la Ziwa Victoria na maeneo mengine katika kaunti 46.

Dkt. Gikungu amesema mvua hizo ambazo tayari zimesababisha maafa ya watu na mifugo na uharibifu wa mali, zitaendelea kwa siku mbili kuanzi leo Ijumaa hadi Jumapili.

Kaunti zilizotajwa kuwa huenda zikaathiriwa na mvua hizo kubwa ni pamoja na kaunti za Mombasa, Taita Taveta, Tana River, Kilifi, Lamu, Kwale, Wajir, Garissa, Mandera, Marsabit na Isiolo.

Kaunti nyingine ni pamoja na kaunti za Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu, Tharaka-Nithi, Nairobi, Machakos, Kitui, Makueni, Kisumu, Homabay, Siaya, Migori miongoni mwa kaunti nyingine za Magharibi mwa Kenya.

Dkt. Gikungu vile vile amewatahadharisha wakazi wa maeneo hayo kwua waangalifu kwa uwezekano wa mafuriko, upepo mkali, na ongezeko la mawimbi baharini katika nyanda za Pwani.

BY MJOMBA RASHID

Mwisho.