HabariNews

WANANCHI WAHIMIZWA KUJIHUSISHA NA AINA TOFAUTI TOFAUTI ZA UKULIMA

Wakazi wamehimizwa kujihusisha na aina tofauti tofauti za ukulima ili kujikwamua kutoka kwenye lindi la umasikini ambao umekuwa ukiwakabili. Changamoto ya wakulima wengi kushindwa kujiendeleza maishani ikitajwa kuwa kujihusisha na upanzi wa mmea aina moja. Kilimo kikiwa miongoni mwa nguzo muhimu zinazoshikilia uchumi wa mataifa mengi duniani, mbinu zinazotumika kufanya ukulima huo zimetajwa kuchangia kufaulu kwa wakulima au kusalia katika hali ya uchochole.

Mbunge wa Kilifi kaskazini Owen Baya amewashauri wakazi kaunti ya Kilifi na ukanda wa pwani kwa jumla, kubadilisha mfumo wa ukulima wa mmea aina moja kwa wakati ambao wamekuwa wakiendeleza kwa muda mrefu na badala yake waanze kupanda mimea tofauti tofauti kwa wakati mmoja.

Ameeleza kuwa hatua hiyo itawasaidia wakulima kupata vyakula vingi kwa wakati mmoja ambapo wanaweza kujipatia pesa wanapouza mavuno hayo pamoja na kujipatia lishe bora. “Unapata chakula na unapata vitu vyengine vya kuuza unaendesha maisha. Na mimi nawashukuru kwa ile bidii ya kilimo mnafanya lakini mnafanya kilimo aina moja pekee mnapanda mahindi pekee. Na hilo shamba unalolima sasa ukipanda mahindi, ufuta, njugu, ukiweka muhogo hutahitajika kulima mara mbili. Na sisi hapa Kenya ndio tunauwezo wa shamba kupanda kila kitu tofauti na mahali kwengine ambapo wanalima aina moja pekee kwa wakati lakini hapa kwetu kwasababu ya hali ya hewa inakubali kila aina ya mimea.” alisema Baya.

Hata hivyo amewasistiza wakazi kukumbatia ukulima kutokana na ubora wa hali ya hewa ukanda wa pwani, jambo analodai kuwa linasaidia katika kupata mavuno mengi.Amefichua kwamba kando na elimu kuwa njia ya kujitoa katika umasikini, ukulima ndio njia rahisi ya kumpa mtu kipato, huku akieleza kuwa hiyo ndio sababu kubwa iliyompelekea yeye kuwasilisha miswaada katika bunge la kitaifa ya kutaka kutambuliwa kwa mimea ya mkorosho na mnazi kuwa miongoni mwa mimea muhimu humu nchini. “Mimi sijui ikiwa mnanielewa ninachosema? Ndugu zangu kuna njia za kutengeneza pesa. Ni sisi tuamue tuupige teke huu umasikini. Mimi naamini vitu viwili ndugu zangu elimu na ukulima umaskikini unatoka ndio mimi mnaniona nakazana sana na mambo ya mikorosho, mnazi na mambo ya pamba. Na sasa tushafungua mtambo wa muhogo  na huo mtambo endapo hatutapanda muhogo ule mtambo utafungwa na ule mtambo unaweza kuajiri watu wengi lakini lazima muhogo upandwe”. alisema Baya.

Ikumbukwe mbunge wa Matuga Kassim Tandaza aliwasilisha bungeni mswaada wa kutaka mmea wa BIXSA maarufu mrangi kutambuliwa kama miongoni mwa mimea muhimu humu nchini kama vile kahawa na majani chai.

ERICKSON KADZEHA.