HabariNews

Ripoti ya upasuaji wa mwili wa Joseph Ochieng Anyaa imeonyesha kwamba alifariki dunia baada ya kutokwa na damu nyingi ndani ya kichwa.

Ripoti ya upasuaji wa mwili wa Joseph Ochieng Anyaa aliyepatikana amefariki dunia katika njia tatanishi kwenye kituo cha polisi cha Changamwe mjini Mombasa imeonyesha kwamba alifariki dunia baada ya kutokwa na damu nyingi ndani ya kichwa.

Upasuaji huo uliofanywa na mwanapatholojia Ngali Mbongo kwenye hospitali ya rufaa ya Coast general unaonyesha kwamba hali hio ilisababisha uharibifu wa ubongo.

Imearifiwa kuwa Ochieng mwenye umri wa 32 ambaye ni baba wa watoto watano alipatikana amefariki dunia siku ja jumamosi iliyopita asubuhi katika seli ya kituo hicho ambako alikuwa anazuiwa baada ya kupatikana akiiba.

Ochieng amedaiwa kushambuliwa na kundi la watu wenye ghadhabu na kumpiga baada ya kupatikana akiiba vifaa vya magari katika gereji moja eneo la Kwahola usiku wa ijumaa iliopita tarehe 30, baadaye kundi hilo lilimpeleka kwenye kituo hicho cha polisi.

Aidha madai mengine yalioibuliwa ni kwamba Ochieng alikuwa amelewa alipowasilishwa kwenye kituo hicho, hata hivo alipelekwa kwenye hospitali ya Portrieze kutibiwa kisha akarejeshwa kwenye kituo hicho kabla ya kugunduliwa ameenga siku ya jumamosi asubuhi.

Watu kadhaa wanaushukiwa kumpiga Ochieng wamekamatwa.

BY EDITORIAL TEAM