HabariNews

Halmashauri inayoshughulikia kampuni za bima nchini yatakiwa kuhakikisha kampuni zinaweka kiwango maalumu cha malipo kwa jamii ya watu wanaoishi na uwezo maalum.

Jamii ya watu wanaoishi na uwezo maalum kaunti ya Kwale wameitaka halmashauri inayoshughulikia kampuni za bima nchini kuhakikisha kampuni zinaweka kiwango maalumu cha malipo kwa jamii hio ili kuwapa uwezo wa kukata bima.

Wakiongozwa na christine Jefwa anayeishi na ulemavu wa ngozi, anasema kwamba jamii hio inakumbwa na changamoto nyingi za kimsingi ambazo zinawanyima nafasi ya kulipa ada za bima kama binaadam wengine.

Kwa upande wake Mwalimu Ali mshirikishi wa watu wanaoishi na uwezo maalum ameahidi kutoa hamasa ya bima kwa jamii hio ili waweze kupata fidia wakati wanapokumbwa na mikasa.

Hata hivyo kwa upande wake afisa wa halmashauri ya kuthibiti utendakazi wa kampuni za bima nchini Evan’s Kibagendi amesema kwamba tayari swala hilo linajadiliwa ili kuona kwamba kila mkenya anapata nafasi ya kuekeza katika bima.

Huku hayo yakijiri, muungano wa madalali wa bima nchini AIBK umeelezea hofu ya kudodora kibiashara endapo haitatilia maanani utumizi wa teknologia ya kisasa kuuza bima katika ulimwenguni wa kibiashara.

Mwenyekiti wa muungano huo Antony Mwangi anasema kwamba teknologia imewezesha kampuni nyingi kufikia idadi asilimia kubwa ya wateja nchini na hata mataifa ya nje na kurahisisha kuimarika kwa biashara zao.
Akizungumza katika kongamano la 16 la kutathmini na kujadili changamoto zinazokumba biashara ya bima nchini linalofanyika huko Diani kaunti ya Kwale, Mwangi amesema kwamba tayari wanaendeleza mazungumzo na kampuni za bima ambazo zilizopiga marufuku baadhi ya magari humu nchini ili kuona kila mmiliki wa magari anapata bima kwa kila kampuni.

BY EDITORIAL DESK