HabariLifestyleMombasaNews

Serikali ya Kaunti ya Mombasa Yaapa Kukabiliana Vikali na Visa vya Dhuluma za Kijinsia.

Mikakati maalum itawekwa kukabiliana na ongezeko la dhuluma za kijinsia kaunti ya Mombasa.

Akiongea wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Ukoaji wa Waathiriwa wa Dhulma za Kijinsia huko Maunguja eneobunge la Kisauni, Gavana wa Mombasa Abuldswamad Sheriff Nassir ameapa kukabiliana na visa vya dhuluma za kijinsia kwa kuhakikisha sharia inawakabili wanaoendeleza visa hivyo.

Akikemea vitendo hivyo Nassir amesema kuwa serikali yake itabuni kitengo maalum cha kuhakikisha kuwa kinafuatilia kwa kina dhuluma hizo kuhakikisha kuwa wahusika wanaadhibiwa vilivyo.

“Tutaunda team kuangalia na kujua kila ambaye amedhulumiwa, tutajaribu kuweka team ili watu wapate uwakilishi katika Korti mtu afungwe mpaka chupa ioze iwe funzo kwa wengine,” akasisitiza Nassir.

Gavana huyo aidha amewashtumu wanaoendeleza unyama huo na kuwataka kukoma mara moja  akisisitiza kuwa ni ukiukaji wa haki za kibinadamu.

“Hakuna mwanamume wa kisawaswa anayeweza kuinuka na kuangalia skati au mtoto mdogo asiyeweza kujitetea ukamnajisi. Wewe si mwanamume! Haya mambo lazima yakome kwenye jamii yetu,” Akasema Gavana Nassir.

Waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Jaji Mkuu Martha Koome, Jaji wa mahakama ya Mombasa Olga Sewe, Hakimu mkuu katika Mahakama ya Mombasa Martha Mutuku miongoni mwa viongozi wengine.

BY NEWS DESK.