HabariNews

Wakazi Watishia Kuandamana Kulalamikia Kero la Ndovu Kilifi

Wakaazi wa eneo la Mwangea Kwa Dadu eneobunge la Malindi Kaunti ya Kilifi wametishia kuandamana kutokana na uvamizi wa ndovu kwenye mashamba yao.

Wakazi hao wamelalamikia uharibifu wa mimea yao huku mtu mmoja akiripotiwa kufariki.

Wakaazi hao wamewataka viongozi waliwachagua kuchukua hatua kali dhidhi ya uvamizi huo ambao umewasababishia hasara kubwa kwenye mashamba yao ambayo kwa sasa yana vyakula.

Matatizo ya huku ni ndovu wanaingia shambani wanakula mahindi, mikunde wanaharibu kila kitu, wanakuja saa kumi na moja jioni wanatoka saa tisa alfajiri, tunawafukuza hawatoki,” wakasema wakazi.

Mkaazi mwengine mwenye hasira naye akaongeza haya, “mahali imefikia itabidi tuchukue hatua, tuandamane maana tuliowapigia kura hatuoni msaada wao.”

Itakumbukwa kuwa lalama za wakazi hao zinajiri licha ya Shirika la Wanyamapori nchini KWS kubaini kuweka mikakati kabambe ya kudhibiti mizozo baina ya binadamu na wanyamapori katika maeneo yaliyoathiriwa kaunti ya Kilifi.

Mkurugenzi mkuu wa KWS kaunti ya Kilifi John Wambua alidokeza kuwa wamefungua vituo tamba vyenye askari wa kukabiliana na kuwafurusha ndovu karibu na makazi ya wananchi.

“Mgogoro wa wanyamapori na binadamu umeongezeka, lakini kama KWS tumefungua mobile units. Bamba tuna mobile units 2, Vitengeni 1. Kando na askari tumekuwa tukitumia ndege kuwafukuza ndogo.” Alibaini Afisa huyo.

Bw. Wambua aidha aliwashauri wananchi kushirikiana nao kwa kupiga ripoti maafisa wa KWS badala ya kuwafukuza ndovu wenyewe.

BY EDITORIAL DESK