HabariNews

Furaha Tele Ndege za Kimataifa Kurejelea Safari za Moja kwa Moja Mombasa

Hatua ya Serikali kufungua anga ya Kaunti ya Mombasa kwa safari za moja kwa moja kwa ndege za Kimataifa hadi Uwanja wa Moi mjini Mombasa imetajwa kuwa itaimarisha biashara na utalii eneo la Pwani.

Seneta maalum wa UDA Kaunti ya Mombasa Miraj Abdillahi amepongeza hatua hiyo akisema italeta maendeleo na kuimarisha sekta mbalimbali ikiwemo viwanda, utalii na biashara.

“Naipongeza serikali yangu ya Kenya Kwanza ni yenye kusikiza maslahi ya mwananchi na kutimiza ajenda zake.” Akasema Miraj.

Miraj ambaye awali katika bunge la Seneti aliibua maswali kuhusu Kufungiwa safari za kimataifa za ndege kwa Uwanja wa Kimataifa wa Moi amebainisha kuwa kufungiwa kwa ndege hizo kulikotaka na janga la Korona kama njia ya kupunguza kuenea kwa ugonjwa huo.

“Tarehe 24 Mwezi wa nne mwaka huu niliuliza masuala tata bungeni ya kwa nini anga ya Moi International Airport ilikuwa imefungwa kwa baadhi ya ndege za kimataifa. Nashukuru baada ya suala hilo kuliibua na kufuatiliwa ilibainika kuwa safari hizo zilisimamishwa kwa sababu ya janga la Covid-19 wakati huo,” Alisema Miraj.

Seneta huyo maalum aidha amepongeza juhudi za serikali kufufua uchumi wa Pwani kwa miradi mbalimbali ya kimaendeleo, akiitaja ziara ya rais William Ruto eneo la Pwani kuwa ziara ambayo ilifanikisha kufunguliwa tena kwa anga la Mombasa kwa ndege za kimataifa.

“Pongezi sana kwa rais wetu, ndege hizo zitaleta wawekezaji kwa mradi wa uchumi wa Dongo Kundu, itawarahisishia watalii pia hivyo niwasihi vijana wadumishe amani kwa ajili ya maendeleo zaidi,” akakariri Miraj.

Itakumbukwa kuwa mnamo mwezi Apirili 2023 seneta Miraj aliwasilisha hoja bungeni kwa kamati ya fedha na bajeti bungeni akitaka sababu kwa nini ndege za kimataiafa kuzuiliwa katika uwanaja wa ndege wa kimataifa Mjini Mombasa.

Katika waraka wake bungeni Miraj alitaka kamati hiyo itoe sababu kwa nini Wizara ya Uchukuzi ilifutilia mbali na kuondoa leseni ya ndege za moja kwa moja ya mashirika ya kimataifa yakiwemo Shirika la ndege la Uturuki na Qatar, kutua Mjini Mombasa, huku akiihimiza serikali kurejesha mfumo wa anga wazi (Open sky policy) ili kuvutia uwekezaji wa kimataifa na kuimarisha sekta ya utalii.

“Nimesimama hapa kutaka taarifa kwa nini haki za kutua kwa ndege kadhaa za Kimataifa zimeondolewa na kunyimwa haki hiyo Uwanja wa Kimataifa wa ndege wa Moi mjini Mombasa. Nataka kamati ya bunge ieleze kwa nini hilo na ieleze Bunge hili la Seneti mikakati iliyowekwa kupambana na athari zilizojitokeza baada ya kusitisha safari hizo za ndege,” Alisema Miraj.

Wadau mbalimbali wa masuala ya uchumi, utalii na biashara nao walieleza Kufurahishwa na hatua hiyo wakisema kuwa kuna uchumi wa ukanda wa Pwani utakua na kuimarika japo si kwa haraka sana, lakini ni hatua chanya.

BY MJOMBA RASHID