HabariLifestyleMazingiraNews

Zingatieni Usalama wa Wanafunzi NTSA Yaonya Wenye Magari Ya Shule

Mamlaka ya Kudhibiti Usafiri na Usalama barabarani NTSA imetoa onyo kwa madereva wa magari yanayosafirisha wanafunzi dhidi ya kuyaendesha magari kiholela ili kuepuka ajali mbaya za barabarani.

NTSA imewataka madereva wazingatie sheria za barabarani huku ikiahidi kuchukua hatua kali kwa dereva yeyote atakayekiuka sheria hizo ikiwemo kuwapokonya leseni zao za udereva.

Mkurugenzi wa mikakati ya usalama barabarani Samwel Musumba ameomba usimamizi wa shule mbalimbali nchini kuhakikisha kuwa shule zinafungwa mapema ili kuwaruhusu wanafunzi kurudi nyumbani kwa ajili ya likizo katika wakati ufaao.

“Wahudumu wote ambao magari yao yatapatikana na makosa ya ukiukaji sheria kama Mamlaka tutawachukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria. Lazima tuwalinde watoto wetu hawa tuhakikishe wanafika nyumbani, na shule zihakikishe zinafunga mapema ili watoto wafike makwao mapema,” akasisitiza Bw, Musumba.

Aidha Mkurugenzi huyo alisema ni sharti magari yakaguliwe kabla kuwabeba wanafunzi huku akisisitiza kuwa usimamizi wa shule unafaa kuhakikisha madereva wao wana ujuzi wa kutosha barabarani ili kuepuka visa vya ajali.

“Tunahimiza Uongozi wa shule kuhakikisha kuwa magari yao yako imara na hali nzuri kubeba wanafunzi, pia ijadiliane na madereva kujua iwapo wapo hali salama na utulivu wa kuyaendesha magari ya shule.” Alisisitiza Bw. Musumba.

Ikumbukwe kuwa kumesalia wiki moja kabla ya kukamilika kwa muhula wa 2 wa masomo na hatimaye shule kufungwa na wanafunzi wakitarajiwa kusafiri kurejea majumbani mwao.