HabariNews

NACADA Yatoa Siku 14 Kubaini Uhalisi wa Aina Mpya ya Mihadarati

Mamlaka ya Kitaifa Kudhibiti Utumizi wa Dawa za Kulevya na Pombe nchini NACADA imetoa taarifa kuhusu video zinazosambaa mtandaoni kuhusu uvumbuzi wa aina nyingine ya mihadarati.

Mamlaka hiyo kupitia Kaimu Mkurugenzi wake Bw. John Muteti imesema bado haijabaini kiini cha dawa hiyo akiongeza kuwa huenda uvumbuzi wa dawa hiyo ni mchanganyiko wa dawa nyingine za kulevya.

Akiongea na wanahabari mjini Mombasa Jumanne Agosti 8, Muteti amesema kuhusu kanda za video zinazosambaa mtandaoni bado haijabainika iwapo kanda hizo ni za hapa nchini akiwataka Wananchi kuwapa muda wa siku 14 ili kufanya uchunguzi wa dawa hiyo.

“Tumeona video ambazo zinasambaa kwenye mitandao zikionyesha watu wakiwa kwenye hali ambayo si nzuri kutokana na hilo tuko hapa kujua ni dawa gani kwa sababu hata sisi bado hatuna taarifa kuhusu dawa hii na lazima tupate taarifa kamili ili tujuze wananchi kuhusu kinachoendelea.” Alisema Mutetei.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Reach Out Centre Taib Abdulrahman alisema tatizo la mihadarati limefikia hatua nyingine ambayo watumizi huchanganya mihadarati na dawa tofauti tofauti zinazouzwa katika maduka ya dawa za rejareja.

“Tumeona tatizo la utumizi wa mihadarati unaingia ukingo mwingine, tumeona wanaenda kuchanganya dawa za tiba na dawa nyingine na mara nyingi hizi ni ambazo zinauzwa katika maduka ya reja reja ya kuuza dawa lakini katika tathmini zetu mpaka sasa hatujaona ongezeko la kutumia mihadarati kupita kiwango.” Alisema Bw. Abdulrahman.

Naye Mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu kutoka Shirika la MEWA Hussein Taib alirai vitengo mbali mbali kuwahamasisha wanajamii kuhusu dawa za kulevya vile vile akirai vyombo vya habari kuwa mstari wa mbele katika kuelimisha jamii ili kuepukana athari inayokodolea macho taifa.

“Kitu ambacho naomba hata nyinyi wanahabari hii kazi msiachie serikali ama mashirika ya kijamii, naomba tushirikiane fanyeni utafiti ili mweze kuhamasisha jamii kuhusu athari ya dawa ya kulevya,” alisema Bw. Hussein.

Itakumbukwa kuwa eneo la Pwani liliorodheshwa la pili katika matumizi ya mihadarati na la kwanza katika matumizi ya pombe miongoni mwa vijana, kwa mujibu wa utafiti uliotolewa na shirika la NACADA mnamo mwezi Juni 2023.

BY EDITORIAL DESK