HabariNews

Tutashiriki Mazungumzo na Upinzani Kwa Masharti, Rais Ruto

Serikali ipo tayari kushiriki mazungumzo ya maridhiano na mrengo wa Upinzani, lakini kwa masharti.

Akiongea Jumatatu, Agosti 7 huko eneobunge la Mukurweini kwenye ziara yake ya Mlima Kenya Rais William Ruto alisisitiza kuwa ni sharti mazungumzo hayo yasihusu suala la ushirikiano maarufu ‘handshake.’

“Kwa sababu mumekubali mambo ya handshake mumewachana nayo mimi jambo la pili pia tukubaliane mambo ya vita na fujo na kuharibu mali na biashara ya watu pia na hiyo tukubaliane tukomeshe katika taifa letu la Kenya.” Alisema Rais.

Rais Ruto aliutaka upinzani uachane na mpango wa maandamano kabla ya mazungumzo hayo yaliyoratibiwa kufanyika Jumatano wiki hii, akibani kuwa iwapo watakubaliana masharti hayo mawili basi serikali haitasita kuzungumza na upinzani kujadili masuala mengine.

“Ikiwa tutakubaliana kwa mambo hayo mawili kwamba hakuna handshake na hakuna vurugu then we can proceed as a country, we can discuss the rest of the things (basi tutasonga mbele kama nchi na kujadiliana masuala mengine),” akasisitiza rais Ruto.

Kwa upande wake naibu wa rais Rigathi Gachagua na Kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Kimani Ichungwa waliunga kauli ya rais wakisisitiza kuwa hawatajadili maswala mengine kando na yale matano ambayo waliyaweka wazi.

“Tungetaka kuomba kwa heshima kwa sababu umekubali Kimani Ichungwa aongoze mazungumzo na sisi tunamuamini Ichungwa akiwa hapo tumewakilishwa, lakini kabla uanze mazungumzo tunakuambia kabla uanze hii mzungumzo uweke sharti kwa Raila Odinga na timu yake kuwa lazima waachane na vurugu kabisa katika mambo ya siasa,” alisema Gachagua.

Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichungwa alieleza kuwa amewasiliana na kiongozi wa AZIMIO kwenye mazungumzo hayo, Kalonzo Musyoka na kukubaliana mazungumzo hayo kufanyika sehemu ya hadharani kuanzia saa tano unusu asubuhi siku hiyo ya Jumatano.

“Nimeongea na makamu wa rais wa zamani Kalonzo Musyoka leo na nimemuambia kuwa tumekubaliana Jumatano saa tano unusu asubuhi tutaonana, lakini tunataka tukutane eneo la umma kama pale Bomas of Kenya na tunataka kamera kwenye mkutano ili atueleze na kila Mkenya asikie,” alikariri Ichungwa.

Aidha serikali ya Kenya Kwanza imesema kwamba haitajadili suala la gharama ya juu ya maisha akisema kuwa tayari serikali imeweka mikakati ya kuzalisha chakula cha kutosha nchini.