HabariNewsSiasa

IPOA yapendekeza Kubuniwa kwa Ofisi ya Kiongozi wa Upinzani

Mamlaka ya Kutathmini Utendakazi wa Polisi IPOA imependekeza kubuniwa kwa ofisi ya Kiongozi wa Upinzani.

IPOA ambayo Jumatano Septemba 27, ailiwasilisha mapendekezo yake mbele ya kamati ya maridhiano katika ukumbi wa Bomas iliibua wasiwasi wake kuhusu ghasia na machafuko yanayoshuhudiwa nchini kila baada ya uchaguzi.

Kulingana na Mwenyekiti wa IPOA Anne Makori, iwapo Ofisi ya Upinzani itabuniwa na sera kabambe kuwekwa itakuwa hatua mwafaka ya kudhibiti ghasia na mizozo inayopelekea maafa.

Ofisi rasmi ya Upinzani ni muhimu sana sababu ikiwa kuwa kila kipindi cha uchaguzi mkuu tunapata vurugu na ghasia hapa nchini na tunaona vifo vinashuhudiwa na inaleta mtafaruku mwingine, tunajua sote. Masuala ya sheria za uchaguzi yanaweza kushughulikiwa katika afisi ya upinzani na wapewe mfumo mwafaka wa kukabiliana na serikali bila fujo wala maafa,” alisema Bi. Makori.

Makori aidha aliitaka kamati hiyo ihakikishe maabara ya uchunguzi ya DCI iwe huru ili kupunguza ushawishi wa polisi huku ikifichua kuwa ripoti zinazotolewa kwao na polisi hufadhiliwa na maafisa wanaowachunguza hatua ambayo imetajwa kuathiri utendakazi wao.

Kwa upande wake Kamishna wa IPOA Moreen Muthaura alisema Mamlaka hiyo inapendekeza kuongezewa mamlaka ya kuendesha mshtaka ili kukabiliana na visa vinavyohusu utendakazi wa polisi, sawia na kuepukana na ucheleweshwaji wa haki.

“Iwapo IPOA itapewa mamlaka ya kuendesha mashtaka, Mamlaka hii itaweza kuharakisha uchunguzi wake si kwa lengo hasa la kuwaadhibu maafisa wa polisi lakini kuhakikisha kuwa mchakato wa uchunguzi na uendeshaji wa kesi pia unakuwa wa haraka vilivyo,” alisema.

BY MJOMBA RASHID