HabariNewsSiasa

‘Tulilazimishwa kujiuzulu!’ Waliokuwa makamishna wa IEBC wadai Chebukati alikiuka sheria, Uchaguzi Mkuu 2022

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC Wafula Chebukati alifanya maamuzi kadhaa peke yake pasi kushirikisha makamishna wenza.

Ni kauli yake Francis Wanderi mmoja wa waliokuwa makamishna wa IEBC alipokuwa mbele ya kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo ya Maridhiano, mnamo siku ya Alhamisi Septemba 28.

Waliokuwa makamishna wa IEBC Justus Nyang’aya na Francis Wanderi walikuwa wamefika mbele ya Kamati hiyo kutoa mapendekezo yao matano wanayotaka kushughulikiwa.

Akizungumza kwenye kikao cha Kamati hiyo katika ukumbi wa Bomas, Wanderi alidai kuwa Chebukati alipuuza uamuzi ulitolewa na mahakama kuhusu mamlaka yake, na kwamba alichagua maafisa wachache wa IEBC na kuwahusisha kwenye majukumu yaliyopaswa kutekelezwa na makamishna.

“Samahani kusema hivi kuwa Mwenyekiti wa IEBC hakufuata uamuzi ule wa mahakama ya Upeo unaopatikana katika kesi ya 2017 IEBC vs Maina Kiai na wengine, Mwenyekiti aliamua peke yake akishirikiana na baadhi ya wafanyakazi wa IEBC ambao aliichagulia mwenyewe alifanya hivyo kinyume cha Katiba na kwa kukiuka sheria,” alisema Wanderi.

Akiunga mkono kauli yake, Justus Nyang’aya naye alidai kuwa ushauri wake na ule wa baadhi ya makamishna ulipuuzwa wakati wa maandalizi na wakati wa uchaguzi na hasa kusitishwa kwa kiwambo cha kupeperusha matokeo.

“Mwenyekiti peke yake aliamua kuchukua uamuzi wa kuinyima nchi nafasi ya kujumlisha matokeo kulingana na matokeo yaliyoorodheshwa kama hakikisho la picha zilizowasilishwa na matokeo yaliyoitangazwa katika vituo vya kujumlisha matokeo maeneo bunge na Kituo cha kitaifa cha kujumlisha matokeo.

Hili lilisitishwa kama Tume hatukujua uendeshaji wa matokeo haya, na watu majumbani waliokuwa wakifuatilia na kufanya hesabu zao pamoja nasi nao walipote na hawakujua kitu,” Alisema Nyang’aya.

Makamishna hao aidha walidai kuwa walilazimishwa kujiuzulu katika Tume hiyo.

Makamishna wengine wawili ambao ni Irene Masit na aliyekuwa naibu mwenyekiti wa IEBC Juliana Cherera walikosa kuhudhuria moja kwa moja laikini waliwasilisha maoni yao kwa njia ya mtandao.

NA MJOMBA RASHID