HabariLifestyleNewsSiasa

Kenya@60: Rais Ruto asifia juhudi zake za kukwamua uchumi Kenya ikiadhimisha miaka 60 ya Uhuru

Kenya imeadhimisha miaka 60 ya uhuru na kujitawala, maadhimisho ya mwaka huu yakijiri katika kipindi cha msukosuko wa kiuchumi na kupanda kwa gharama ya maisha.

Maadhimisho hayo ya Jumanne, Desemba 12, 2023, yalikuwa yameibua hamu na dukuduku kubwa kwa Wakenya waliozingongwa na ugumu wa maisha na Uchumi, wakitaka kubaini jinsi rais angetegua kitendawili cha kupanda kwa gharama za maisha.

Rais Rais William Ruto ambaye aliongoza maadhimisho hayo ya kitaifa Bustanini Uhuru jijini Nairobi, amekiri kuwa taifa halijafanikiwa kushusha gharama ya maisha akisema bado vijana wengi wamekosa kazi, mapato ya taifa yangali chini.

Hata hivyo rais aliahidi kuwa serikali iatafanya kila juhudi kuhakikisha gharama ya maisha inashuka kwa Mkenya wa kawaida.

“Tumelazimika kutoa mchango wetu katika mapambano ya uhuru wa kiuchumi wa taifa.  Tumelazimika kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi na kuahirisha utekelezaji wa programu muhimu za maendeleo ili kuleta utulivu wa uchumi wetu,” alisema.

Kiongozi huyo wa taifa alisifia hatua zilizopigwa na Serikali yake katika kuimarisha Uchumi, akisema kuwa Uchumi wa taifa umepiga hatua na kuimarika vilivyo katika kipindi cha miezi sita ikilinganishwa na hapo awali.

Kulingana na Rais serikali yake imedhibiti uchumi kwa kushusha mfumko wa bei kutoka asilimia 9.2 hadi 6.8 katika kipindi cha mwaka mmoja.

“Mfumuko wa bei sasa umefikia asilimia 6.8 chini kutoka kiwango cha juu cha asilimia 9.2 mwaka jana,” alisema.

Aidha Ruto aliongeza kuwa kwa kipindi cha muda wa miezi sita sasa mapato ya taifa yamekuwa kwa asilimia 5.4 hali ambayo imeorodhesha taifa kuwa nafasi ya 29 katika mataifa yanayokuwa na Uchumi unaokua, kulingana na Benki ya Dunia.

“Hakuna swali kuhusu hilo: Tulichofanya pamoja, bei ambayo tumelipa pamoja na kujitolea kumeokoa nchi yetu kutoka kwa janga la kiuchumi,” Rais Ruto alisema.

Na licha ya wengi kuwa na kiu cha matumani kuhusu iwapo rais angeangazia mikakati ya kupungua kwa gharama ya maisha, rais hata hivyo amewahakikishia Wakenya kuwa taifa li salama katika hatari ya malimbikizi na shinikizo la madeni.

Ruto amesifia mikakati mwafaka iliyochukuliwa na kuwekwa na serikali yake kuwa juhudi za zililizozaa matunda na zinazotoa hakikisho la kuimarika kwa Uchumi wa taifa.

“Mabadiliko haya ya kiuchumi yalianza na sisi sote kufanya maamuzi na kujitoa mhanga kwa michango mikubwa ya kulikwamua taifa katika shinikizo kuu la deni. Ukubwa wa kujitolea na uzalendo wa Wakenya umejionyesha wazi katika mwaka uliopita na inazaa matunda,” alisema Rais

Rais aliahidi pia kufikia mwezi Januari mwaka ujao hakuna mgeni yeyote atakayehitajika kuwa na visa kuzuru hapa nchini.

Alibainisha kuwa mfumo wa kidijitali umetengenezwa ili kuhakikisha kuwa wasafiri wote wanaokuja Kenya wanatambulika mapema kwenye jukwaa la kielektroniki, akiongeza kuwa wasafiri wote watapata idhini ya usafiri wa kielektroniki.

 

“Haitahitajika tena kwa mtu yeyote kutoka pembe yoyote ya dunia kubeba mzigo wa kuomba viza kuja Kenya,” alisema Rais Ruto.

 

Rais Ruto aliyasema hayo katika bustani ya Uhuru, Nairobi, alipoongoza taifa katika kuadhimisha miaka 60 tangu Kenya iwe jamhuri.

 

BY EDITORIAL