HabariLifestyleMombasaNewsSiasa

Afueni ya Jamhuri Dei! Gavana Nassir alipia ada wagonjwa na kuachia huru wafungwa

Huku taifa la Kenya likiadhimisha miaka 60 ya uhuru, kaunti ya Mombasa iliadhimisha siku hiyo kwa njia spesheli ambapo Gavana wa kaunti ya Mombasa Abdulswamad Sheriff Nassir alitembelea taasisi mbali mbali ikiwemo hiospitali na jela.

Gavana Sharif Nassir aliongoza zoezi la kuwatoa wagonjwa walioshindwa kulipa gharama ya matibabu katika hospitali Kuu Ukanda wa pwani maarufu Makadara.

Kwa mujibu wa Nassir ni kwamba serikali ya kaunti hiyo itagharamikia tiba kwa wagonjwa wote waliolemewa na mzigo wa ada za matibabu.

Akizungumza na wanahabari katika maadhimisho ya sikukuu ya Jamhuri Gavana Nassir alitaja idadi ya wagonjwa watakaotolewa ni 46, huku akitoa agizo kwa familia zilizoshindwa kulipa ada za miili ya wapendwa wao katika mochari kukabidhiwa miili kwenda kuizika.

“Hii leo kwa watu wetu wa Mombasa ambao wameshindwa kulipia bili zao wote waweze kutolewa. Katika hospitali hii (Makadara) ni watu 46 waliokuwa na bili zilizowashinda na nimeagiza dr. Kandwalla aangalie wale walio mochari waruhusiwe ili familia zao waweze Kwenda kuwazika,” alisema Nassir.

Kadhalika aliwataka wawakilishi wadi wote kaunti hiyo kuzuru vituo vya afya vya mashinani na kuwatoa wagonjwa hususan maeneo ya Port Reiz, Tudor na Mrima.

“Nimetoa amri kwa wahehsimiwa wa maeneo wadi waende kwa facility zetu mashinani maeneo yao waangalie wale wenye madeni huko watolewe hasa hospitali za Tudor, Port Reitz na Mrima.” Alisema Gavana Nassir.

Wakati huo huo Gavana Nassir aliagiza waliolipiwa ada hiyo kutoka kaunti ya Mombasa wasajiliwe katika bima ya afya iwapo hawana ili kuepukana na changamoto za ukosefu wa fedha pindi wanapohitaji huduma za afya siku za mbeleni.

“Nimemuagiza Afisa Mkuu wa afya kuwa wale watu wakiwa wanatolewa wasitolewe tu hivi hivi wachukuliwe malezo yao na wapatiwe bima ya afaya ya NHIF haraka iwezekananvyo, tumekuweko tukaweza kuwasaidia kesho tutakuwa hatuko lakini kila kiu kitalipwa.” Alisema Gavana.

Awali gavana Nassir amewalipia faini wafungwa 18 wa makosa madogo madogo na kuruhusu kutolewa katika magereza mbalimbali yakiwemo Jela Baridi, Shimo la Tewa na Annex. Amesema hatua hiyo ni muhimu kwani wengi wamesalia korokoroni kutokana na kushindwa kulipa faini walizotozwa mahakamani.

Ni hatua iliyoungwa mkono na kupongezwa na Mbunge wa Jomvu Badi Twalib akiitaja kuwa ya kipekee na ya kupigiwa mfano huku akihimiza viongozi kushirikiana kuendeleza taifa.