HabariNews

Wakenya sasa kulipa ada za huduma katika E-citizen

Serikali kupitia wizara ya fedha imetangaza kuwa Wakenya watahitajika kulipa ada ili kupata huduma za serikali kupitia jukwaa la E-citizen.

 

Katika notisi yake kwenye Gazeti rasmi la Serikali Waziri wa Fedha Prof. Njuguna Ndung’u amesema wote wanaotaka kupata huduma kwenye jukwaa hilo watahitajika kulipa ada ya usimamizi kwa kila shughuli.

Haya ni kufuatia msingi wa agizo la serikali kwamba wizara zote zinapaswa kuzingatia na kuhamasisha wananchi kuhusu uhamishwaji wa huduma zote za serikali kwenye jukwaa la E-citizen kufikia tarehe 31 Desemba 2023.

 

Hatua hiyo ikiwa ni mojawapo ya mipango ya serikali kuleta mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma za serikali nchini.

 

Wakenya sasa watahitajika kulipa Shilingi 5 hadi 25 kwa huduma zote zisizozidi shilingi 1000 na shilingi 50 kwa huduma ambazo zitawagharimu zaidi ya shilingi 1000.

Hata hivyo Wakenya wamehimizwa kukumbatia matumizi ya mtandao huo wa E-citizen wanapotaka huduma za kiserikali ili kuwapunguzia mahangaiko na gharama wanapotaka huduma hizo.

BY NEWSDESK