HabariNews

Wamiliki wa Matatu wahimiza Madereva kutopandisha nauli msimu huu wa Sherehe

Chama cha Wamiliki wa Matatu nchini M.O.A, kimewataka madereva kutopandisha nauli katika msimu huu wa sherehe za Krismasi na Mwaka mpya.

Chama hicho kimetoa pendekezo hili kikiwasihi madereva kuwa na utu na kuonyesha nia njema kwa Wakenya kutokana na na kuzongwa na gharama ya juu ya maisha.

Akihutubia wanahabari siku ya Jumamosi, Mwenyekiti wa wa Kitaifa wa chama hicho cha Wamiliki wa Matatu, Albert Karakacha aliwasihi wanachama wenzake kuwa waangalifu zaidi wanapotoza nauli kwa abiria wao na kuhakikisha kuwa abiria hawapati usumbufu.

“Tumewataka wanachama wote kuwa makini wanapotoza nauli, tutakuwa tukifuatilia kuhakikisha abiria hawanyanyasiki na kukandamizwa,” alisema.

Karakacha aidha alibaini kuwa katika mwaka mpya wataungana kuhoji kwa nini bei ya mafuta nchini imekosa kupungua vilivyo licha ya kuwa bei za kimataifa zinaimarika na kurudi chini.

Mwenyekiti huyo vile vile aliwataka madereva kuzingatia usalama na sheria za barabarani ili kuhakikisha usalama wa kila mmoja.

“Tunataka madereva wazingatie sheria kwa msingi wa usalama barabarani ili kuhakikisha abiria wetu wanafika salama wanakoelekea wakati huu wa msimu wa Krismasi,” alisema Karakacha.

Wakati uo huo aliwataka maafisa wa polisi hasa wale wa trafiki kutotumia nguvu na kukoma kuwangaisha na kuwanyanyasa madereva wanaposimamia usalama wa barabarani.

BY MJOMBA RASHID