HabariNews

Walimu wa Shule Sekondari Msingi waapa kutorejea Shuleni Mwaka Ujao

Walimu wa shule za Sekondari msingi (Junior Secondary) wameapa kutorejea shuleni mwezi Januari hadi pale matakwa yao yatakaposhughulikiwa.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari mapema leo mchana viongozi wa kitaifa wa walimu hao wamesema Tume ya Huduma ya Walimu, TSC na Wizara ya Elimu zinapanga kuwapa kandarasi nyingine ya mwaka mmoja baada ya sasa kukamilika Disemba 31 mwaka huu.

TSC na Wizara ya Elimu hazipaswi kuongeza kandarasi nyingine kwa kuwa iliwekwa wazi katika kipepengee cha 4 kuwa mkataba huo ulikuwa ni kandarasi ya mwaka 1 isiyoweza kuongezwa. Walimu walioko kwenye mafunzo ya kandarasi hizo (Intern teachers) hawapaswi kuongeza kandarasi hizo hata wakihujumiwa au kutishiwa na Maafisa wa TSC wa kaunti ndogo,” walisema.

Kulingana nao, TSC na Wizara ya Elimu zinakiuka matakwa na makubaliano yao kwa kuwa walimu hao walipaswa kuhudumu kwa kandarasi ya mwaka mmoja pekee kisha waajiriwe kwa mkataba wa kudumu.

Daniel Muriithi ambaye ni Katibu Mkuu wa Muungano wa walimu hao, amesema walimu kamwe walimu hawatakubali tena kuhudumu kwa kandarasi huku wakilalamikia mazingira magumu katika shule hizo.

Kandarasi zinaisha Disemba 31, 2023. Hatutafika shuleni Januari 2024 hadi iwe kwa mkataba wa kudumu na vigezo vya uhakika,” alisema Murrithi.

Wakati uo huo viongozi hao wameikosoa kauli ya rais William Ruto kuwa serikali imeajiri walimu 56,000 wakiitaja kama kauli ya uongo wakisema kuwa ni walimu 10,000 ambao wameajiriwa kwenye mkataba wa kudumu.

Uongo uliotolewa na rais William Ruto ni hujuma ya juu sana na utovu wa nidhamu wa hali ya juu kwa kuwa Serikali haijaajiri walimu 56,000 lakini imeajiri walimu elfu 10 pekee kwa mkataba wa kudumu na idadi ya walimu elfu 46 iliyobakia ni walimu walioko kwenye kandarasi ya muda ya mkataba wa mafunzo kazini (internship) ya mwaka mmoja, kandarasi ambayo si ya kuongezwa,” alisema Bw. Murrithi.

Hatua hiyo yao ya kususia kuripoti shuleni mwakani inatazamiwa kulemaza shughuli za elimu na kuwa pigo kubwa kwa mtaala wa umilisi, CBC.

Ikumbukwe kuwa mahakama iliamuru kesi ya walimu hao dhidi ya TSC na Wizara ya Elimu isikilizwe mwezi Machi mwaka ujao.

BY MJOMBA RASHID