HabariNews

Rais Ruto akutana na Mawazziri Kuidhinisha Utumizi wa TSA

Baraza la Mawaziri limeidhinisha utekelezwaji wa mfumo wa Akaunti moja ya Fedha za Serikali maarufu TSA mfumo utakaotumika na Serikali Kuu na zile za Kaunti.

Katika kikao cha Baraza la mawaziri kilichoongozwa na rais William Ruto siku ya Jumatatu, Baraza lilisisitiza umuhimu wa mfumo huo katika kurahisisha huduma za benki za serikali, kubuni njia za serikali kuhakikisha uwazi katika usimamizi wa pesa za serikali na raslimali.

Akiongea katika kikao hicho Rais Ruto alisema mfumo huo mpya utasaidia kudhibiti matumizi na kupunguza mgawanyiko wa akaunti za serikali katika benki za biashara ili kuhakikisha kuwa fedha zinazoingia na kulipwa na wananchi zinaingia katika sehemu moja.

 “Fedha za Serikali huwekwa kwenye akaunti za benki za biashara na watu binafsi huendelea kupata riba. Hii lazima ikome. Manufaa yote ya fedha za umma lazima yawafikie watu wa Kenya pekee na si mtu mwingine yeyote.”

Mfumo huo mpya utasaidia serikali kuondoa suala la serikali kuwa na akaunti nyingi za benki ambapo hapo awali kila idara ya serikali ilikuwa na akaunti mbalimbali za kupokea fedha zilizolipwa kwa njia ya simu kwa huduma tofauti tofauti raia walizokuwa wakilizipia.

Muuondo wa TSA utajumuisha akaunti ya Hazina ya Kitaifa, Akaunti Ndogo ya TSA na Hazina ya Mapato ya Kaunti.

Wakati uo huo baraza la mawaziri pia liliidhinisha utekelezwaji wa Ununuzi wa Kielektroniki wa Serikali (e-GP) katika serikali za Kitaifa na za Kaunti, hatua ambayo imepania kuimarisha haki, usawa, uwazi, ushindani na ununuzi wa umma kwa bei nafuu.

Rais Ruto alirejea katika Ikulu ya Nairobi baada ya kuwa nje ya Nairobi kwa takribani muda wa wiki mbili na kuongoza kikao hicho cha baraza la mawaziri kilichohudhuriwa na mawaziri na makatibu wote pamoja na naibu wa rais Rigathi Gachagua.

Katika picha zilizosambazwa na Idara ya mawasiliano ya Ikulu zilionesha mandhari mapya na kuashiria mabadiliko kutokana na ukarabati wa kihistoria uliofanywa ili kuiboresha Ikulu hiyo iliyodumu kwa miaka 100.

Ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, Baraza la
Mawaziri liliidhinisha Mfumo wa Dhamana ya Kijani wa Kenya ambao
unalenga upatikanaji mbadala wa fedha za ufadhili kwa uwekezaji wa
kijani wenye ukakamavu kufuatia ongezeko la gharama za mabadiliko ya tabianchi.

Baraza la Mawaziri pia liliidhinisha rasimu ya Sera ya Kenya ya Ulinzi
wa Jamii ya 2023 ambayo inalenga kuwaepusha maskini na wasio kuwa na uwezo kutokana na changamoto za kijamii na kiuchumi. Sera hii inawiana na mamlaka ya kikatiba na malengo ya maendeleo ya taifa, ikisisitiza
umuhimu wa ulinzi wa kijamii katika kupunguza umaskini na ukuaji
shirikishi.

Ajenda zingine zilizoidhinishwa na Baraza la Mawaziri ni Sera ya
Utambuzi Awali wa Mafunzo, Kuanzishwa kwa Kituo cha Msaada wa Kisheria cha Afrika na Mkataba wa Kujiunga na Benki ya Uwekezaji ya Miundombinu
ya Asia.

BY NEWSDESK