HabariNews

Gachagua Arudi Nyuma! Asitisha mpango wa Kumshatki Jaji Esther Maina

Naibu wa Rais Rigathi Gachagua sasa amesitisha na kubadili nia yake ya kutaka kuwasilisha malalamishi yake mbele ya jaji mkuu Martha koome dhidi ya jaji Esther Maina.

Gachagua anayetaka jaji huyo atolewe ofisini mara moja kwa madai ya ufisadi alifutilia mbali mpango wake huo ili kupisha mazungumzo ya Idara hiyo ya Mahakama na Serikali Kuu.

Katika taarifa kutoka kwa ofisi ya Naibu wa Rais hatua hiyo ilichangiwa na kuwepo wito wa kuruhusu mazungumzo baina ya Serikali Kuu na Idara ya Mahakama kujadili mienendo ya maofisa wa idara hiyo.

Gachagua amesema aliipokea taarifa ya hatua Jaji Mkuu Martha Koome kutoa nafasi ya mazungumzo baina ya serikali kuu na idara hiyo, wito ambao rais Ruto aliukumbatia na kuukubali.

Kulingana na Afisa wa huduma za mawasiliano katika afisi hiyo Njeri Rugene, Gachagua amechukua hatua hiyo ili kupisha mdahalo kati ya Viongozi wa Serikali Kuu, Idara ya mahakama na washikadau wengine wa asasi za serikali ili kutatua mzozo wa madai ya ufisadi katika idara ya mahakama unaotokota kwa sasa.

Naibu wa Rais amekuwa akisisitiza alihujumiwa na jaji Esther Maina kinyume cha sheria na alikuwa ameapa kumfungulia mashtaka jaji huyo ili kuchunguzwa kwa kina na Tume ya huduma za mahakama JSC kwa misingi ya ufisadi na mienendo isiyofaa kama afisa wa mahakama nchini.

Itakumbukwa siku ya Jumatatu jaji mkuu Martha Koome aliitisha kikao na Rais ili kujadili tofauti zilizopo na madai ya ufisadi yanayozingira idara kuu za serikali, wito ambao umepingwa vikali na chama cha mawakili nchini LSK na viongozi wa Upinzani akiwemo Kinara wa Azimio Raila Odinga.

BY NEWS DESK