HabariNews

Rais Ruto akutana na CJ Koome Ikuluni

Serikali ya Kenya Kwanza hatimaye imeafiki kuzingatia utawala wa sheria, uhuru wa Kitaasisi na kuheshimu kikamilifu maamuzi ya Mahakama.

Katika Mkutano uliofanyika Ikulu ya Nairobi na kuleta Idara zote Kuu za Serikali ikiwemo Bunge na Idara ya Mahakama, mnamo siku ya Jumatatu, Rais William Ruto alitoa hakikisho kuwa idara hizo kuafiki kushirikiana katika kutekeleza majukumu yao pasipo kuingiliana uhuru wao.

Katika kile kilichoonekana kutuliza joto na mvutano wa hivi majuzi baina ya Serikali Kuu na Idara ya Mahakama mkutano huo wa Jumatatu Januari 22, ulilenga kuunda mikakati ya kupambana na ufisadi, kuimarisha uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa Wakenya.

Serikali Kuu, Bunge na Idara ya Mahakama zimeafiki kila idara binafsi kuunda sera, kanuni na mapendekezo ya kisheria ili kufikia malengo ya kupambana na ufisadi, kuimarisha utoaji huduma na uwajibikaji wa kitaasisi wa Idara zote za Serikali kwa Wakenya,” ilisoma taarifa kutoka kwa Msemaji wa Ikulu Hussein Mohammed.

Kwenye kikao hicho pia Idara zote ziliafikiana kuunda sera na kushirikiana kuendesha majukumu yao kwa kuheshimu uhuru wa kila idara na utawala wa sheria na kwamba suala la ufisadi ni Donda sugu linalolemaza shughuli zote na maendeleo ya nchi.

Na ili kuhakikisha kunakuwa na utoaji huduma mwafaka na kupambana na ufsadi, Serikali Kuu pamoja na Bunge ziliafiki kuunga mkono ombi la Idara ya Mahakama kupata nyongeza ya mgao wa bajeti ili kufanikisha kuajiriwa kwa majaji 25 wa Mahakama Kuu na majaji 11 wa Mahakama ya Rufaa sawia na raslimali kukamilisha mpango wa kukodisha magari ili kukidhi mahitaji ya usafiri ya mahakama.

BY MJOMBA RASHID