HabariNews

Kaunti Kupata Mgao zaidi wa Fedha, Rais atia saini Nyongeza ya Bilioni 46.3

Rais William Ruto ameidhinisha hatua na nia ya serikali yake ya kuongeza mgao wa fedha za serikali za kaunti.

Rais Ruto ametia sahihi kuwa sheria mswada wa nyongeza za fedha za serikali kaunti wa mwaka 2023 unaolenga kuongeza serikali za magatuzi shilingi bilioni 46.

Hatua hiyo itawezesha serikali za kaunti kupata nyongeza ya shilingi bilioni 46.3 za mwaka 2023/2024 huku akiahidi kuwa serikali ya kitaifa itaendelea kutoa rasilimali kwa serikali za kaunti ili ziendeleze shughuli zake vyema.

Akizungumza katika Ikulu ya Nairobi Ruto alibainisha kuwa kati ya fedha hizo shilingi bilioni 5 zitatumika katika usambazaji wa mbolea ya bei nafuu na shilingi bilioni 4.5 kugawanyiwa kaunti 18 kutekeleza mpango wa maeneo ya viwanda.

Vile vile shilingi milioni 454 zitatolewa kwa kaunti tano ikiwemo Lamu na Tana River ili kujenga makao makuu ya maeneo hayo.

Haya yanajiri kufuatia Baraza la Magavana, CoG kuendelea kushinikiza mgao wa fedha wa shilingi bilioni 450 katika mwaka wa kifedha 2024/2025.

BY NEWSDESK