HabariLifestyleNewsSiasa

Rais Ruto Ataka Muda wa Ulipaji Deni kwa Mataifa ya Afrika Kuongezwa hadi Miaka 50

Rais William Ruto ametoa wito wa kuwepo haja ya kurekebishwa sera zilizopo za ulipaji deni kwa mataifa ya ukanda wa Afrika Mashariki.

Rais amedai sera zilizopo za ulipaji madeni zinakandamiza na kuumiza mataifa ya Afrika Mashariki kuhusiana na ulipaji wa deni.

Akizungumza Jumanne wakati ufunguzi wa kikao cha tatu cha Bunge la Afrika Mashariki (EALA) katika majengo ya bunge jijini Nairobi, rais Ruto alisema muda mfupi wa ukomavu wa deni ndio imechangia sababu kuu nchi nyingi katika ukanda huu zinaendelea kukabiliwa na madeni.

Amesema ili kuruhusu mageuzi imara ya kiuchumi katika eneo hili kunahitajika kuwa na nyongeza ya muda wa ulipaji deni la mkopo wa maendeleo kutoka miaka 3 hadi 10 na aidha mkopo wa deni la miaka 15 kuongezwa muda wa ulipaji hadi miaka 50.

“Ongezeni muda wa ulipaji wa fedha zilizokopeshwa kwa maendeleo kutoka miaka 3 hadi pengine miaka 10. Lazima tuongeze muda wa deni kwa maendeleo ya raslimali kutoka miaka 15 hadi pengine kati ya miaka 40 na 50.” Alisema.

Rais alidai hatua hiyo ni kuyapa mataifa muda wa kutosha kukusanya raslimali kwa ajili ya maendeleo na kutekeleza miradi ya maendeleo pasi vikwazo vya kulipa deni hilo.

BY MJOMBA RASHID