Serikali ya kaunti ya Kilifi imehimizwa kuongeza madaktari wanaohudumu nyanjani ili kuboresha afya ya jamii ya watu wanaoishi na uatilifu. Hatua hii inafuatia kubainika kuwa wengi wa jamii ya watu wanaoishi na uatilifu wamekuwa hawapati huduma za matibabu kwa wakati kutokana na changamoto za kufika hospitalini.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa jamii ya watu wanaoishi na uatilifu kaunti ya Kilifi Jacob Sirya, mikakati ikiendelea kuwekwa ili kuhakikisha kwamba kila mkaazi kaunti ya Kilifi anapata huduma bora za matibabu, wito umetolewa kwa serikali ya kaunti ya Kilifi kuharakisha mpango wa kuwasajili watu wote wanaoishi na uatilifu ili iweze kubainika ni huduma gani za kiafya wanazohitaji.
Anasema, jamii hiyo imekuwa ikinyimwa haki ya matibabu bora kutokana na changamoto ya umbali wa sehemu wanakoishi, huku akieleza kuwa hatua ya kuwasajili itarahisisha mikakati ya kuwajumuisha kwenye mpango wa bima ya kitaifa ya matibabu.
Aidha ameeleza matumaini yake kuwa mpango huo utafanikiwa na jamii ya watu wanaoishi na uatilifu wataweza kufikiwa na madaktari wa nyanjani kama vile wenzao kutoka kaunti jirani ya Mombasa baada ya gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro kuwaahidi kuiunga mkono hoja hiyo.
BY ERICKSON KADZEHA.