HabariLifestyleNews

Maafa ya watoto Shakahola yatawala maadhimisho ya mtoto wa Kiafrika nchini.

Kenya imeungana na mataifa mengine barani kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kiafrika huku serikali ikihimizwa kumlinda mtoto wa kiafrika dhidi ya athari zote hasa za itikadi za kidini.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ikiwa ni haki ya mtoto katika mazingira ya kijiditali, maadhimisho haya hapa nchini yakijiri katika kipindi ambacho watoto wamehusika na mkasa wa maafa ya Shakahola.

Hapa Pwani Mashirika ya kutetea haki za binadamu eneo la Pwani yamejumuika familia za waliopoteza watoto wao katika msitu wa Shakahola ili kuwakumbuka wana wao walioaga dunia kupitia mkasa huo.

Wahaharakati wa kutetea haki za kibinadamu wameishinikiza serikali kuendeleza uchunguzi wa kina kubaini kiini cha yaliyojiri Shakahola.

Hussein Khalid ni Mkurugenzi mkuu wa HAKI Afrika ameonyesha kufadhaishwa na matukio ya Shakahola, “Tumehuzunishwa sana na yaliyotokea Shakahola, watoto kuathirika na hata kupoteza maisha yao, serikali ilikuwa wapi? Hakuna cha kuadhimisha siku hii iwapo familia za watoto hao hazijapata haki,” akasema Bw. Khalid.

Hata hivyo kulingana na mwenyekiti wa Mamlaka Kutathmini huduma za Polisi, IPOA, Ann Makori amesema kuwa hakuna afisa wa serikali ambaye atasazwa katika uchunguzi huo.

Kauli zao zimeungwa mkono na Mesaid Omar msimamizi wa miradi kutoka shirika hilo kuwa kuna haja ya serikali kuhakiksha  inamlinda mtoto wa Kiafrika kutokana na athari zote hasa za itikadi za kidini akitolea mfano maafa ya Shakahola yaliyojumuisha watoto.

Huku hayo yakijiri Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za watoto la Compassion International Samwel Mwabogo ameeleza haja ya watoto kulindwa dhidhi ya taarifa zenye madhara wanazopata kupitia mitandao.

Mwabogo anasema japo mfumo wa kijiditali una manufaa yake hasa katika kuendeleza masomo karne hii ya 21 kuna mengine ambayo yanaweza kudhuru watoto mitandaoni.

Hata hivyo amedokea kuwa shirika hilo linawahamasisha watoto nchini kuhusu jinsi ya kutumia mitandao kwa manufaa yao.

Maadhimisho haya yaliyoasisiwa na Umoja wa Afrika OAU mnamo mwaka elfu moja mia tisa tisaini na moja (1991) hufanyika kila mwaka tarehe 16 mwezi Juni ili kuwakumbuka watoto zaidi ya mia moja waliuawa na maafisa wa usalama huko nchini Soweto Afrika kusini mwaka 1976 walipokuwa wakiandamana kulalamikia kutengwa kielimu, ubaguzi wa rangi na ukoloni.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka  huu ikiwa ni haki ya mtoto katika mazingira ya kijiditali.