HabariNews

Waliookolewa Shakahola wadaiwa kushiriki ngono

Ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma, ODPP imewasilisha ombi la
kuwataka watu waliokolewa msitu wa shakahola kaunti ya Kilifi kuhamishwa
hadi gereza la Shimo la Tewa kaunti ya Mombasa.
Hii ni baada ya Serikali kuibua wasiwasi kuwa huenda kukashuhudiwa mimba
zisizotarajiwa hasa baada ya ripoti kuibuka kuwa wanajihusisha na ngono
kutokana na watu hao kukaa mahali pamoja.
Naibu Mkurugenzi wa mashtaka ya umma Jami Yamina amesema ombi hilo
linafuatia hofu ya serikali kuwa huenda ikalaumiwa kwa kuchangia mimba
zisizohitajika miongoni mwa wanawake.
Akiwa mbele ya Hakimu mkuu wa mahakama ya Shanzu, Joe Omide, Yamina
amesema hali ya afya ya 65 hao imeaimarika hivyo wanaume wanapaswa
kutenganishwa na wanawake na kuwekwa katika vituo tofauti gerezani Shimo
la Tewa.
Yamina amesema kwamba waathiriwa hao wamekuwa wakitangamana hasa
wanapokula na wanapokuwa kwenye chumba ambako wamekuwa wakilala pamoja.
Ikumbukwe walikamatwa baada ya kutokea mauaji ya wafuasi halaiki katika
msitu huo, yaliyohusishwa na mhubiri tata Paul Mackenzie ambaye angali
kizuizini.

BY EDITORIAL DESK