HabariNews

Vikundi 39 vya Usimamizi wa Fuo za Bahari Mombasa Kunufaika na Milioni 111

Makundi ya Usimamizi wa Fuo za Bahari-BMUs yanatarajiwa kufaidika kupitia fedha kutoka kwa serikali ya kaunti ya Mombasa zinazolenga kuimarisha sekta ya uvuvi na uchumi samawati.

Gavana wa Mombasa Abdulswamad Sheriff Nassir ametangaza kuwa serikali ya kaunti imetenga shilingi milioni 100 ili kuwezesha makundi hayo.

“Na hivi tunavoongoea tumeweka milioni 111, hii pesa haitatumika kwa vikundi vingine vyovyote, itatumika kwa BMUs peke yake vikundi tulirejesta Cooperatives za BMU pekee ili waweze kununua neti zaidi na maboti na wawe na revolving fund kuendeleza kazi zao,” akasema Gavana Nassir.

Akizungumza wakati wa Hafla ya awamu ya pili kufadhili vikundi hivyo huko Jomvu, Gavana Nassir ameipongeza wizara ya uvuvi wa uchumi samawati kwa kuweka rekodi ya malengo yake kwa wakati ufaao.

Nassir aidha amepongeza makundi hayo kwa kujiunga katika vyama vya ushirika akisema kuwa hatua hiyo itarahisisha ugavi wa fedha hizo na kuhakikisha kuwa kila kikundi kinafaidika vilivyo na mpango huo.

Wakati uo huo Nassir ameahidi kuzindua kituo cha utoaji mafunzo ya masuala ya uchumi samawati ili vijana wapate ujuzi wa kutosha katika sekta hiyo.

“Tunataka vijana wetu waanze kusoma mambo ya uchumi samawati, tutakuwa na sekta yetu yenyewe ili vijana wetu wasitoke hapa kwenda South Afrika, Dar e salaam kwa nini? Kwani bahari yetu ina chumvi aina gani ya kwamba hatuwezi kusomesha watoto wetu sisi tukiwa hapa.” Alisema Nassir.

Kibibi Abdallah ambaye Waziri wa Uchumi wa Uchumi Samawati amepigia upatu hatua ya ufadhili wa vikundi hivyo akitaja kuwa itainua zaidi maisha ya familia nyingi hasa zile zinazotegemea biashara za uvuvi.

Kibibi alisema mpango ni miongoni mwa ajenda kuu za Gavana Nassir kuboresha uchumi wa kaunti.

BY MJOMBA RASHID