HabariNews

Upinzani Kuja na Mfumo Mpya wa Maandamano, Asema Odinga

Kinara wa Mrengo wa Azimio Raila Odinga ameitaka Jumuiya ya Kimataifa kujitokeza na kukashifu ukiukaji wa haki za kibinadamu baada ya watu kuuwawa kufuatia maandamano ya upinzani.

Akizungumza Siku ya Ijumaa Agosti 11 wakati wa ibada ya misa ya walioaga dunia wakati wa maandamano huko Bondo kaunti ya Siaya, Odinga alisema kuwa vitendo vya maafisa wa usalama viliashiria unyanyasaji kwa baadhi ya wananchi kupitia mkondo wa uongozi akimtaka rais William Ruto kuwajibishwa kufuatia matukio hayo.

“Tunaitaka Jamii ya Kimataifa kusimama na Kenya, tunaskitika kwamba Jumuiya ya kimataifa imenyamazia ukatili na hata haki za msingi za Wakenya zikikandamizwa,” alisema Odinga.

Odinga aidha alikashifu makaribisho ya Kiongozi wa mashtaka katika mahakama ya ICC aliyewasili nchini ili kutuzwa na Chuo Kikuu cha Mt. Kenya akidai hatua hiyo ni haikuwa sawa hasa ikizingatiwa kuwa maakama hiyo inapaswa kusimamia haki.

“Kiongozi wa Mashtaka wa ICC alikuwa hapa na alipokelewa na kulakiwa na Bw. Ruto Ikulu na kupewa helkopta kwenda kupokea digrii, tunasema hii si sawa ICC lazima isalie kuwa huru na aminifu kwenye jukumu lake,” alikariri Bw. Odinga.

Wakati huo huo Odinga amedokeza kwamba maandamano yataendelezwa katika siku zijazo japo kwa njia mbadala ambapo waandamanaji hawataelekea kwenye maeneo ya umma.

“Wakati mwengine hatutawaambia watu waingie barabarani kuandamana, tutawaambia wakae majumbani, Kaeni majumbani na tuone watafanya nini. Tutawaambie msitoke nje, na mzuie kila mmoja atakayetoka….iko njia mingi ya kuua paka,” akasisitiza Odinga.

Kwa upande wake Kinara NARC Kenya Martha Karua ameshikilia kuwa Mrengo wa Azimio haumtambui Rais William Ruto kama kiongozi hadi pale atakapokubali kufungua Seva za IEBC na kuthibitisha ushindi wake.

Aidha Karua amesitiza kuwa kinara wa Azimio ndiye aliyeshinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

“Ruto anatafuta kutambulika ati ndio akikohoa tuwe tunanyamaza sote mimi nataka kumwambia hatuwezi kumtambua kwa sababu ya kuua bindadamu, tutamtambua wakati seva itafunguliwa sababu sisi Wanaazimio tunajua aliyechaguliwa ni Raila Amollo Odinga,” alisema Karua.

 BY EDITORIAL DESK