HabariLifestyleNews

Kitendawili cha Taifa: Idadi ya Waliosajiliwa kwa Mradi tata wa Sarafu ya Worldcoin haijulikani

Ofisi ya Kamishna wa Kulinda Data (ODPC) imefichua kuwa idadi ya watu ambao walisajiliwa kwenye mradi tata wa sarafu ya Worldcoin bado haijulikani, kwa sasa.

Kamishna wa data Immaculate Kassait ametoa ushahidi mbele ya Kamati ya idara ya Mawasiliano Habari na Ubunifu akisema kuwa ODPC imeanza kuchunguza ili kubaini hali halisi ya utendakazi wa Worldcoin pamoja na kubaini taarifa sahihi iliyokusanywa na mradi huo.

“Mnamo April 19 2022, ODPC ilimwandikia barua Mkurugenzi mkuu wa WorldCoin ikitaka taarifa za ukusanyaji wa data muhimu za kibinafsi hasa kimsingi wa sharia ya ukusanyaji na usafirishaji wa data binafsi, uthibitisho wa kukubali usafirishaji wa data miongoni mwa taarifa nyingine,” Kassait aliiambia kamati.

Aidha Kassait ameongeza kuwa bado haijatambulika ikiwa kampuni hiyo imekuwa ikifanya kazi ndani ya mifumo ya kisheria licha ya kampuni hiyo kumiliki cheti cha usajili.

“Cheti hakimaanishi kuwa kampuni inajulikana na ODPC kuwa inasindika data za watu nchini Kenya,” alisema.

Haya yanajiri baada ya serikali kusimamisha shughuli zote zinazohusiana na mradi wa crypto kwa sababu za kiusalama.

Ikumbukwe kuwa Mawaziri wa Usalama wa ndani Prof. Kithure Kindiki, na mwenzake wa Teknolojia na Mawasiliano Eliud Owalo wanatarajiwa kufika bungeni kwa mara nyengine tena Jumatano hii ya Agosti 16 kujibu maswali kuhusu kampuni hiyo ya sarafu na usalama wa data za Wakenya.

Hii ni baada ya wawili hao kushindwa kujieleza kikamilifu wiki jana kuhusu uwepo kwa kampuni ya Worldcoin nchini.

Na Mjomba Rashid