HabariLifestyleNews

Nuru Gizani? Mzozo wa Ardhi ya Kazamoyo-Samburu Kupata suluhu ya Kudumu

Kamati ya Ardhi katika Bunge la Kaunti ya Kwale imeahidi kutatua mzozo wa umiliki wa ardhi ya ekari elfu 22 uliopo baina ya wakazi wa Kazamoyo huko Samburu na bwenyenye mmoja.

 

Inaarifiwa kuwa mzozo huo umedumu kwa muda mrefu sasa baina ya wakazi hao na bwenyenye huyo anayejihusisha na upanzi wa makonge katika mashamba yanayodaiwa kuwa ya wenyeji.

Spika wa bunge la Kwale Seth Mwatela na mwakilishi wa wadi ya Puma, James Dawa, wamesema kuwa kamati hiyo itafanya uchunguzi wa kina ili kutafuta suluhu ya mzozo huo ambao umewaathiri zaidi ya wakaazi elfu 15 kwa muda mrefu sasa.

“Katika zile ardhi ambazo ziko na utata ni wakati serikali saa hii inatakikana kuja kuangalia na ifanye survey,” akasema Bw. Mwatela.

“Sisi tumekuja kama bunge kuja kushirikiana na wananchi wetu kusikiliza je vilio vyao ni nia gani ambazo tunaweza kuvitatua ili tupate suluhu la kudumu ili wananchi wa Kazamoyo waishi kama wakenya wengine wowote,” akaongeza Bw. Dawa.

Aidha, viongozi wa bunge hilo wameshtumu vikali hatua ya maafisa wa polisi wa GSU wanaodaiwa kuwapiga na kuwajeruhi vibaya baadhi ya wakaazi waliokuwa wakipinga unyakuzi wa ardhi yao na bwenyenye huyo siku chache zilizopita.

“Tunaweza kupata kuwa kulikuwa na police brutality kuna wananchi ambao waliweza kupigwa na askari, tutajaribu kuifuatilia ili haki ipatikane,” akakariri Spika huyo.

Kwa upande wao wakaazi walidai kuwa bwenyenye huyo amekuwa akishirikiana na maafisa wakuu wa serikali ili kuwatishia wenyeji kwa kuwatumia polisi wa kitengo cha GSU.

Wakiongozwa na mwathiriwa Umazi Julo aliyedai kupigwa na polisi na mwenzake Sandra Mbithe, wakaazi hao walisisitiza kuwa wao ndio wamiliki halali wa ardhi hiyo.

“Nilipigwa na GSU ambao ni serikali, wamenivunja mkono kwa sababu natetea shamba letu.” Akasema mkaazi mmoja.

Naye mkaazi mwengine alisema, “huyu bwenyenye alikuwa akitunyanyasa sana, amelima mpaka makaburi ya wazazi wetu, mababu zetu mahali walizikwa amekuwa akilima na kupanda makonge juu. Kwa nini asimamiwe na serikali kuharibu mali yetu, kunyakua mashamba yetu?”