HabariNews

Hoja ya kuhalalisha Mazungumzo ya maridhiano kufikishwa Seneti

Licha ya utata na ushindani kuhusu ajenda kuu za mkutano, Kamati ya mazungumzo ya maridhiano baina ya serikali na upinzani imeendeleza mazungumzo hayo Jumatatu ya Agosti 21.

Mazungumzo hayo yaliongozwa na Kimani Ichung’ah wa upande wa Kenya Kwanza na mwenzake wa Azimio la Umoja, Opiyo Wandayi huku wakiwataka wakenya kupuuzilia mbali wanaotilia shaka mazungumzo hayo.

Akizungumza baada ya mazungumzo hayo Wandayi ambaye pia ni mmoja wa wanachama wa Azimio kwenye kamati hiyo, alisema hoja ya kuhalalisha rasmi shughuli za kamati ya mazungumzo ya maridhiano ilipitishwa kwa kauli moja kwenye bunge la kitaifa na itajadiliwa seneti wiki ijayo.

Wandayi aidha amesema siku 60 walizopewa zitaanza rasmi baada ya hoja hiyo kupitishwa na bunge la seneti.

Wakati huo huo Mbunge wa Malindi Amina Mnyazi amesema jopo lililoteuliwa kufanya mazungumzo kati ya mrengo wa Azimio na Kenya Kwanza ni sharti litambuliwe ili mazungumzo hayo yaweze kufaulu.

Mnyazi amesema umuhimu wa kufanya mazungumzo ni kumwangazia mwananchi wa kawaida huku akisisitiza kuwa viongozi wa mrengo wa Azimio wako tayari kupata suluhu ya mambo yanayowaathiri wananchi.

“Umuhimu wa kufanya hili ni kuhakkikisha kuwa mazungumzo katika lile jopo yawe ni mazungumzo ambayo yako na uzito. Na uzito ni kwamba lazima lile jopo litambulike. Tutakuwa tuko na mandate na nguvu ya kutekeleza mambo kadhaa,” alisema Mnyazi.

Haya yanajiri huku Mkutano huo wa Jumatatu Agosti 21 uliofanyika katika ukumbi wa Bomas ukikosa kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa Azimio kwenye mazungumzo hayo Kalonzo Musyoka na kiongozi wa wengi bunge la seneti Aaron Cheruiyot.

Inaarifiwa kuwa wawili hao walitoa udhuru kwani wako ziarani nje ya nchi kwa masuala binafsi.

Huku hayo yakijiri Viongozi wa mrengo wa Azimio one Kenya waliisuta serikali wakisema kuwa hawana haja ya kujiunga na serikali ya Ruto.

Wakiongozwa na kiongozi wa DAP Kenya Eugene Wamalwa huko kaunti ya Bungoma, viongozi hao walisema kwamba cha msingi kwao ni kuhakikisha kuwa matakwa ya kila mkenya yametekelezwa na kupewa kipau mbele ila siyo kujiunga na serikali ambayo imejaa ukabila.

Aidha viongozi hao wamepinga madai kwamba mrengo wao una haja ya serikali ya nusu mkate.

“Hoja yetu kama watu wa Azimio ni kuhakikisha kuwa matakwa ya kila mwanachi yametekelezwa na kuwaambia watu wa kenya kwanza waache kudanganya wananchi kwamba sisi tunataka serikali ya nusu mkate, sisi hatuna haja ya nusu mkate.” alisema Wamalwa.

Kwa upande wake katibu mkuu wa DAP Kenya Dkt. Asal Simiyu amesema kwamba hawatokubali tume ya uchaguzi IEBC kuendesha uchaguzi wa mwaka wa 2027.

“Tunataka kuwaambia kuwa hatutakubali tume ya uchaguzi IEBC kuendesha uchaguzi wa mwaka wa 2027 ikiwa hivi ilivyo.”