Viongozi mbalimbali kutoka ukanda wa Pwani walikutana Alhamisi Oktoba 19 jijini Nairobi kujadili masuala ya maendeleo ya Pwani.
Wakiongozwa na Spika katika bunge la seneti Amason Jeffah Kingi na aliyekuwa Gavana wa Kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho Viongozi hao walisema kikao hicho cha viongozi wa Pwani kililenga kuimarisha umoja wa kimaendeleo.
“Hawa ndio viongozi ambao wamekuja pamoja kuweka vichwa pamoja kujadili masuala ya Pwani hususan masuala ya kimaendeleo, na mazungumzo tumekuwa nayo kwa kina maafikiano tumekuwa nayo kwa ajili ya jamii zetu,” alisema Kingi.
Walidokeza kuwa wameelewana kuweka mikakati thabiti ili kuleta maendeleo eneo la Pwani.
“Tumesema kwamba tutaweka ajenda inayomgusa Mpwani yeyote kimaendeleo na matarajio yetu mahitaji yetu katika serikali ya William Ruto saa hii. Tutakuwa na mazungumzo ya kimikakati mwafaka ya jinsi tutakavyomhusisha na kuafikia maendeleo ya eneo la Pwani,” alisema aliyekuwa gavana wa Mombasa Hassan Joho.
Viongozi hao aidha walipinga suala la ubinafsishaji wa baadhi ya sehemu za Halmashauri ya Bandari ya Mombasa KPA, suala ambalo limeendelea kuzua gumzo na mhemko kote nchini.
Hata hivyo Kulingana na Mchanganuzi wa masuala ya Kisiasa Pwani Maimuna Mwidau licha ya kupongeza muungano huo, alipuuzilia mbali suala la Bandari ya Mombasa kuunganisha viongozi hao ili kuwasilisha matakwa yao kwa rais Ruto, akisema kuwa kuna masuala mengi ya maendeleo yanayopaswa kuangaziwa na si suala la bandari pekee.
Aidha alibaini kuwa viongozi wanaopaswa kuwa mstari wa mbele kuliangazia na kuliwasilisha serikalini suala la Bandari ni mawaziri Aisha Jumwa wa Jinsia na Utamaduni na mwenzake wa Uchumi Samawati, Salim Mvurya.
“Wanaopaswa kuwa mstari wa mbele kuendeleza ajenda, mazungumzo ni mawaziri Mvurya na Jumwa, Spika Kingi hao ndio wako serikalini wanaweza kumfikia na kumshawishi rais zaidi ila kwa hao wengine kuongea nahisi ni kujitafutia umaarufu kisasa,” alisema Bi. Mwidau.
Japo alipongeza hatua ya Muungano huo, Bi. Mwidau aidha alisema haukuwa wakati mwafaka kwa viongozi hao kujitokeza kuunda Umoja huo ikizingatiwa masuala ya uchaguzi yalipitwa na wakati.
Bi. Mwidau alidai kuwa walipaswa kushikana na kuungana mapema hata kabla ya uchaguzi ili kuwa na ushawishi kitaifa.
“Kuja kwao pamoja ni sawa lakini sio wakati mwafaka, walipaswa kufanya hivyo kabla ya uchaguzi tungekuwa na nguvu na usemi katika serikali na kitaifa kama maeneo mengine,” alisema.
Mkutano huo uliowaunganisha viongozi wote hao wa Pwani uliitishwa na Spika wa Bunge la Seneti, Amason Jeffa Kingi.
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria ni Waziri wa jinsia na utamaduni Aisha Jumwa, Waziri wa Uvuvi na Uchumi Samawati Salim Mvurya, magavana wote wa kaunti 6 za pwani, magavana wa zamani, maseneta, wabunge miongoni mwa viongozi wengine.
Walikuwepo pia Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki, EALA Hassan Sarai (UDA) na Suleiman Shahbal (ODM).