HabariMombasaNews

Gavana Aiongoza Mombasa Kupokea Shehena ya dawa Kutoka KEMSA

Kaunti ya Mombasa imepokea shehena ya dawa kutoka kwa Mamlaka ya usambazaji dawa na vifaa vya matibabu nchini KEMSA.

Akizungumza katika hafla hiyo ya kupokea shehena hiyo na uzinduzi wa Mpango wa Usambazaji dawa huko Port Reitz Changamwe, Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir alisema kuwa shehena hiyo itawezesha kuwepo kwa dawa za kutosha katika hospitali zote za kaunti.

Kulingana na Gavana Nassir ujio wa shehena hiyo iliyogharimu kaunti Sh. 60m  itaimarisha mpango wa huduma za afya huku akibaini kuwa fedha zitakazopatikana kutoka kwa malipo ya bima ya NHIF hazitajumuishwa katika mapato ya hazina ya kaunti bali zitatatumika na vituo vya afya kuboresha huduma.

Nassir Aliwahakikishia wakazi wa Mombasa huduma bora za afya katika hospitali zote za kaunti hii ili kupunguza msongamano unaoshuhudiwa katika hospitali ya rufaa ya ukanda wa Pwani, maarufu Makadara.

Ile uboreshaji wa taasisi tulikuwa nayo kitambo, na sasa every facility ile pesa inaingia NHIF haitaenda kwa mapato ya Kaunti itaenda kwa zahanati yenyewe ili ijiboreshe.” Alisema

Gavana Nassir aidha alidokeza kuwa tayari kaunti inabadilisha miundomsingi iwe ya kisasa huku akidokeza kuwa kila hospitali za magatuzi yote madogo ya kaunti ya Mombasa zinafanya kazi kwa saa 24.

tayari mashine ya X-ray tumeiboresha na tutaweza kusimami wenyewe kama kaunti na tutabadilisha miundomsingi ya taasisi zote za afya kwa kaunti ndogo zote za kaunti za Mombasa ziwe zinafanya kazi kwa saa 24.” Alisema Gavana Nassir.

Kinara wa Azimio la Umoja Raila Odinga aliyehudhuria hafla hiyo ya uzinduzi wa dawa hizo ameupigia upato mpango huo huku akiwapongeza magavana wa mrengo wa Azimio kwa kuwajibikia majukumu yao vilivyo.

Muhimu zaidi ni kuboresha huduma kwa wananchi hiyo ndiyo kazi ya serikali za kaunti na mimi nina furaha sana kuona kazi inafanyika. Juzi ile kampuni ya Info Track imefanya maoni Kenya nzima kuangalia huduma, nimeongea na Mkurugenzi wa Infotrack na ameniambia matokeo ya ripoti hiyo imeonyesha magavana wa Azimio wanafanya vizuri zaidi kushinda wale wengine, na hiyo imenifurahisha sana.” Alisema Odinga.

Kauli yake Odinga inajiri baada ya gavana Nassir kuibuka gavana bora katika masuala ya afya kwenye utafiti wa kura ya maoni uliofanywa na shirika la Info track mwezi uliopita.

BY MJOMBA RASHID