HabariNews

Mitihani ya Kitaifa KCSE Yaanza, Serikali yaonya Watumizi wa Mitandao dhidi ya Kuvujisha Mitihani

Mitihani ya Kitaifa kidato cha nne KCSE iliyong’oa nanga leo Jumatatu inaingia siku yake ya 2 Jumanne Novemba 7 kwa mtihani wa Hisabati karatasi ya 1 na kisha baadaye mchana mtihani wa Kiingereza karatasi ya 2.

Mitihani hiyo inaendelea huku mikakati kabambe ya kuhakikisha usalama wa mitihani hiyo ikiwekwa, licha ya wadau na wachambuzi wa elimu kuibua madai na hofu ya udanganyifu.Kutokana na hayo Serikali imeapa haitalegeza kamba katika kuwasaka watu wanaotumia vifaa vya kidigitali kufanya makosa dhidi ya mtihani.

Katibu wa elimu msingi Belio Kipsang alitahadharisha kuwa msako unaoendelea utaimarishwa katika maeneo yanayolengwa katika shughuli hiyo haramu.Kipsang alibaini kuwa wizara yake itaendelea kufanya kazi ya karibu pamoja na wizara ya ICT kuimarisha vipengele vya usalama vya mtihani inayoendelea kutokana na kufichuliwa mapema.

Tutaendelea kuwa imara na kutumia mamlaka yote kwa hawa watumizi wa mitandao ambao wanatupa changamoto kuvujisha mtihani. Tutashirikiana na wenzetu wa Wiozara ya Mawasilainao ICT na DCI kushughulikia uhalifu wa mitandao kuhakikisha kuwa hawa tunawasaka na kukabiliana nao vilivyo, ili mitandao yao tuivunjilie mbali,” alisema Kipsang.

Mitihani hiyo ya kitaifa iliendelea licha ya changamoto ya kutopitika kwa baadhi ya barabara eneo la Pwani kutokana na kuharibiwa na mvua kubwa inayoshuhudiwa nchini.

Kipsanga alitaja maeneo ya Tana River hapa pwani na Turkana kuwa maeneo ambayo athari za mvua ni mbaya ambapo mitihani ililazimika kufikishwa kwa njia ya anga kutumia Helkopta, huku akishinikiza walimu, wanafunzi na wasimamizi wa mtihani kuwa waangalifu wanaposafiri sehemu za mafuriko.

Awali Afisa Mkuu Mtendaji wa tume ya kuajiri walimu nchini TSC Nancy Macharia aliongoza zoezi la ufunguzi wa makasha ya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne KCSE unaoanza leo kote nchini, katika eneo bunge la Mvita kaunti ya Mombasa.

Katika hafla hiyo hata hivyo, Macharia aliwaonya maafisa na wanafunzi watakaopatikana wakijihusisha na visa vya udanganyifu wa mtihani huo watachukuliwa hatua za kisheria. Macharia alisema kuwa walimu wa shule za upili ndio watakaotumika kusimamia mtihani huo huku usamala ukiimarishwa sehemu mbalimbali kunakofanyika mtihani huo.

Leo tumeanza na tunaimani kila kitu kitakuwa shwari, serikali imeweka helkopta tayari kusafirisha mitihani kule kuna changamoto za kiusafiri, kuhakisha kufanikiwa kwa shughuli hii ya mitihani, Walimu na watahiniwa wako tayari pia serikali iko tayari. Mitihani hii itasimamiwa na walimu wa sekondari, na tunahakikisha mafanikio,” Alisema Macharia

Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa elimu ukanda wa Pwani Luka Kangogo alithibitisha idadi ya wanafunzi 52,958 ndio wanaoendelea kufanya mtihani wao wa kitaifa hapa Pwani huku kukiwa na vituo 253 vya mtihani .

Haya yanajiri huku washukiwa 6 tayari wakitiwa mbaroni na kushtakiwa kwa kuhusishwa na matukio ya udanganyifu n uvujishaji wa mitihani ya KCSE inayoendelea.

Sita hao walinsawa kufuatia msako wa makundi mbalimbali ya mitandao ulioendelezwa na maafisa wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini CAK na Idara ya Upelelezi DCI ambao wanafuatilia majukwaa 32 ya mtandao wa kijamii.

By MJOMBA RASHID