Familia moja katika kijiji cha Bangladesh eneobunge la Jomvu kaunti ya Mombasa inaomboleza kifo cha binti yao wa kidato cha 4 aliyefariki baada ya kupigwa na nguvu za umeme.
Mwanafunzi huyo wa shule ya Upili ya Kajembe alikuwa yu njiani akielekea nyumbani baada ya kumaliza karatasi yake ya mwisho ya mtihani wa kitaifa KCSE allipokanyaga waya wa stima na kufariki papo hapo.
Na huko kaunti ya Kilifi, Mjini Malindi katika kijiji ch Kisumu Ndogo huzuni imegubika familia moja kufuatia kuaga dunia kwa mtoto wa umri wa miaka 8 baada ya kutumbukia kwenye shimo la maji taka.
Mtoto huyo anasemekana kufariki alipokuwa akipokea matibabu hospitalini, baada ya kutolewa kwenye shimo hilo, huku wito ukitolewa kwa serikali kusafisha mabomba yote ya kupitisha maji taka ili kuepuka maafa zaidi hasa msimu huu wa mvua nyingi.
Na huko Kisiwani Wasini kaunti ya Kwale familia zaidi ya 6 zimeachwa bila makao baada ya paa na kuta ya nyumba zao kuharibiwa na upepo mkali kutokana na mvua inayoendelea kunyesha.
Ahmed Abubakar ambaye ni mkaazi wa eneo hilo alisema kwamba nyumba takriban 4 zimeharibika zaidi ikiwemo mapaa yake kung’oka na kuta kuporomoka wakati wa tukio hilo lilipotokea.
Kulingana na ripoti kupitia vyombo vya habari ni kwamba hakuna aliyejeruhiwa wakati wa kisa hicho hivyo wakazi hao wameomba serikali na wahisani kujitokeza kuwapatia msaada.
Yakijiri hayo, shughuli za usafiri zikiendelea kutatizika katika barabara kuu ya Likoni-Lungalunga baada ya daraja la Ramisi kufurika maji kutoka na mto Ramisi kuvunja kingo zake.
Abiria wanaotokea maeneo ya Lungalunga na taifa Jirani la Tanzania wamelazimika kusubiri kwa muda mrefu zaidi katika eneo hilo baada ya maji kuziba sehemu hiyo.
Mshirikishi wa Sirika la Msalaba Mwekundu Kaunti ya Kwale Mohammed Mwahenzi alisema kwamba daraja hilo limefurika na kutatiza shughuli za usafiri katika Barabara hiyo.
Madereva wanaotumia Barabara hiyo wameshauriwa kusubiri hadi pale daraja hilo litakaporejea hali yake ya kawaida.
Na huko Kaunti ya Kilifi, Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu nchini KeNHA mnamo Ijumaa ilitoa tahadhari kwa madereva wanaotumia Barabara kuu ya Mombasa-Malindi.
KeNHA inawataka madereva kuwa makini baada ya barabara eneo la Kwa Kadzengo kaunti ya Kilifi Kufurika maji.
Kulingana na KeNHA barabara hiyo kwa sasa haipitiki baada ya kufunikwa na maji kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika eneo hilo na nchi nzima kwa ujumla.
KeNHA iliwaaka madereva kuwa waangalifu wanaposubiri viwango vya maji kupungua kabla ya magari kurejelea usafiri wa kawaida huku eneo hilo likisubiria kufanyiwa ujenzi.
Hata hivyo kwenye taarifa yake KeNHA imedokeza kuwa barabara hiyo mpya itakuwa na urefu wa mita 1.50 zaidi ya iliyopo kwa sasa pamoja na kalvati nne ili kuweka sawa viwango sawa vya pande zote mbili za barabara.
Haya yanajiri huku mvua kubwa zinazoshuhudiwa nchini zikipelekea vifo vya Watu 52 na wengine 56,549 kuathirika kutokana na mafuriko yanayoendelea kushudiwa katika sehemu mbali mbali nchini.
Shirika la Msalaba Mwekundu limetoa ripoti hii baada ya maafa kushuhudiwa katika maeneo tofauti tangu kuanza kwa mvua kubwa nchini.
Ikumbukwe kwamba idara ya hali ya hewa nchini imeeleza kwamba mvua hii inatarajiwa kuendelea hadi Januari mwaka ujao hivyo basi kuzidisha hatari ya uharibifu zaidi.