HabariNews

Makenzie na Washukiwa Wenza Wafika Mahakamani wakiwa Dhaifu kwa Njaa 

Washukiwa wa mauaji ya Shakahola wamekosa kuhudhuria vikao vya kesi dhidi yao licha ya kuwasilishwa katika majengo ya mahakama ya Mombasa mapema Jumanne.

Washukiwa hao akiwemo mshukiwa mkuu Paul Makenzie walishindwa kufika kizimbani kutokana na kudhoofika kiafya baada ya kudaiwa kuendelea kugoma kula.

Wakiwa wamefikishwa mahakamani kwa magari ya polisi baadhi yao walishindwa kushuka katika magari hayo na kulazimika kusaidiwa na polisi.

Afya ya mshukiwa mkuu Paul Makenzie pia ilionekana kubadilika tangu kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo.

Makenzie pamoja na washukiwa hao 94 waliofunguliwa mashtaka 238 ya kuua bila kukusudia, walikuwa wamefikishwa mahakamani kujua hatma yao kubaini iwapo wangeachiwa kwa dhamana au la baada ya Upande wa mashtaka kuiomba mahakama iwazuilie zaidi.

Mojawapo ya sababu kuu ikiwa ni hofu ya washukiwa kuwa katika hatari ya kutoroka iwapo wataachiliwa na kukosa kuhudhuria vikao vya kesi dhidi yao.

Kulingana na upande huo washukiwa walitoroka na kuacha makazi yao hapo awali na kufuata maagizo ya Makenzie ya kufunga hadi kufa, hivyo basi hawawezi kuachiliwa kwa dhamana.

Hata hivyo washukiwa hao ambao walionekana wanyonge kiafya waliwakilishwa na wakili wao Wycliff Makasembo ambaye aliendelea kuwatetea wateja wake hao akisema kuwa upande wa mashtaka hauna sababu za msingi kuendelea kuwazuilia washukiwa hao.

BY MJOMBA RASHID