Kinara wa Azimio la Umoja one Kenya Raila Odinga amemtaka Waziri wa kawi David Chirchir Pamoja na Waziri wa fedha Prof. Njuguna Ndung’u kujiuzulu mara moja.
Hii ni kufuatia madai ya uagizaji mafuta kupitia mkataba wa serikali kwa serikali (G-2-G) ambapo kulingana na Odinga mkataba huo unaojumulisha mataifa ya milki za kiarabu unazidi kuongeza gharama ya maisha ya Mkenya mlipa kodi.
Odinga anasema mkataba huo unawanuafaisha watu fulani serikalini badala ya wakenya wote walipa ushuru na kuwasababishia hali ngumu ya Maisha.
Akiwahutubia wanahabari jijini Nairobi siku ya Jumatatu, Odinga alimkashifu waziri wa kawi na mwenzake wa fedha akisema walishiriki uhalifu na wanapaswa kuondoka mamlakani ili kupisha uchunguzi.
“Bw. Chirchir na Waziri wa fedha Njuguna Ndung’u kwa hakika wamefanya makosa ya jinai, wametumia ofisi vibaya na wakaenda kinyume cha katiba. Waliiba fedha kutoka kwa hazina iliyojumuishwa pamoja na matumizi ya pesa zaidi ya ile iliyoidhinishwa na Bunge. Na si wajiuzulu tu bali pia lazima washtakiwe,” alisema Odinga.
Odinga aidha alisema taifa la Kenya halikuweka mkataba na mataifa ya nje bali mkataba huo ulifanywa baina ya waziri wa kawi na kampuni zinazomilikiwa na serikali katika Mashariki ya Kati.
Haya yanajiri ikikumbukwa kuwa rais William Ruto, Waziri Chirchir na Kampuni za mafuta tayari walikana madai ya Odinga.
Mnamo siku ya Ijumaa, rais Ruto alisema serikali inafanya kila iwezalo kuhakikisha uagizaji wa mafuta unafanyika kwa njia ya uwazi na haki kwa manufaa ya mwananchi.
Alisema Kenya haifanyi kazi kama wakala katika biashara ya ununuzi wa mafuta bali, bali kama mwandishi mdogo anayewajibika kuhakikisha shughuli za mafuta zinafanyika bila matatizo yoyote.
Kwa upande wao Kampuni hizo za mafuta zilishikilia kuwa kulikuwa na Mkataba wa makubaliano uliotiwa saini katika biashara ya mafuta ya Serikali kwa Serikali (G-2-G) na kwamba iliungwa mkono na uwepo wa mahusiano wa biashara ya kimataifa kati ya Kenya na mataifa ya Mashariki ya Kati.
Hata hivyo Odinga amesisitiza kuwa Taifa liko katikati ya utekaji nyara wa serikali na ‘Unyakuzi kamili wa Watu/Mashirika binafsi’