HabariNews

Wakaazi wanaoishi pembezoni mwa mbuga ya Shimba Hills waonywa dhidi ya ukataji miti.

Shirika la kuhifadhi wanyama pori KWS tawi la Kwale limewaonya wakaazi wanaoishi pembezoni mwa mbuga ya Shimba Hills dhidi ya ukataji wa miti jambo liliotajwa kuchangia mabadiliko ya tabia-nchi.

Akizungumza huko Kizibe naibu wa warden wa mbuga hiyo Gilbert Njeru amedokeza kuwa wakaazi wanashiriki sana ukataji wa miti ya mbao hususan miti aina ya M’bambakofi na pia miti ya fito za kujengea hali aliyoitaja kuchangia kukauka kwa chemi chemi za maji mbugani humo.

Afisaa huyo amesema kuwa japo hali ya maisha imegeuka kuwa ngumu kutokana na kiangazi wanatarajia wakaazi kuhifadhi mazingira wala sio kuchangia katika uchafuzi.

Aidha Njeru ameendelea kusema kuwa mbali na miti wanayokata kwa mbao pia wanachoma makaa kwa wingi hali aliyoitaja kuchangia ukame na pia kuua vyanzo vingi vya maji msituni humo ambavyo wanyamapori huvitumia kukata kiu.

Afisaa huyo wa KWS ameweka wazi kwamba ukataji wa miti kiholela unaharibu kabisa makaazi ya wanyamapori hivyo amewataka wakaazi kuacha kabisa ukataji wa miti la sivyo mkono wa sheria utachukua nafasi yake.

BY NEWS DESK