HabariMombasaNews

RAIS AMEZINDUA RASMI KITUO CHA KUUNGANISHA MAGARI KAUNTI YA MOMBASA.

Rais William Ruto amezindua rasmi eneo la uunganishaji magari eneo la Miritini katika eneo bunge la Jomvu kaunti ya Mombasa.

Akizungumza katika uzinduzi huo Raisi Ruto ameelezea matumaini yake kwamba eneo hilo litachangia pakubwa katika kukuza uchumi wa taifa pamoja na ajira kwa vijana.

Uzinduzi wa kituo hicho umeambatana na uzinduzi rasmi wa uunganishaji wa magari aina ya Toyota Fortuner katika kituo hicho.

Kituo hicho kimekadiriwa kugharimu shilingi milioni 130 na kwamba uzinduzi huo  umetajwa na kiongozi huyo wa kitaifa kuwa wa kihistoria kufanyika katika taifa la Kenya.

“Tumekusanyika hapa leo kuweka alama ya mafanikio makubwa katika sekta hii ya uunganishaji wa magari, uchumi na jamii. Tuko hapa kushuhudia uzinduzi mkubwa katika sekta ya viwanda tukisherehekea fursa ya kuzalisha nafasi za ajira na matokeo ya ukuaji wa biashra katika sekta ya viwanda vya magari” amesema rais.

Vile vile Ruto ameongeza kuwa hatua ya uzinduzi wa kituo hicho kutaweka taifa la Kenya kuwa miongoni mwa mataifa yanayokumbatia uwekezaji.

Amewataka wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali wanaopania kutambua kuwa Kenya ina mazingira bora ya kuwekeza.

“ Uzinduzi huu ni Hakikisho kubwa kwa waekezaji  hapa na kote ulimwenguni kwamba Kenya ni eneo lenye thamani kwa uwekezaji ambalo linajivunia kuwa na uaminifu kutoka kwa  biashara kubwa kubwa ulimwenguni.” Amekariri Ruto.

BY EDITORIAL DESK