HabariNewsTechnology

WAKENYA waliokosa Kulipia Husla Fund, Chuma chao Kimotoni

WAKENYA waliokopesha pesa za Hazina ya Hasla na kushindwa kulipia, hawataruhusiwa kupokea mkopo utakaotolewa kwa makundi ili kuwaenua kibiashara.

Kulingana na Rais William Ruto, Wakenya hao watalazimika kulipa madeni wanayodaiwa na hazina hiyo kabla ya kupokezwa mkopo utakaotolewa kwa makundi ya kibiashara.

Rais aliyasema haya akiwa katika eneobunge la Rongai, Nakuru wakati wa kutoa vyeti 1,900 vya ardhi katika maeneo ya Majani Mingi na Lomollo.

“Nafahamu kuwa kuna asilimia kubwa ya Wakenya ambao hawajalipa mkopo wao ila nataka kuwaambia kuwa hawataenda mbali. Tumeongeza pesa ambazo zimetengewa kitengo cha fedha ila hawatapata mkopo huo hadi wakamilishe deni lao,” alisema Rais Ruto.

Hali hii imeibua wasiwasi kuwa idadi kubwa ya Wakenya watakuwa wakiendelea kukopa pesa hizo bila ya kulipa huku serikali ikiongeza Sh10 bilioni zaidi katika hazina hiyo hasaa  katika kitengo kinachojihusisha na biashara.

Mikopo hio ya kibiashara itapeanwa kwa Makundi ya watu 10 au zaidi na wataruhusiwa kupata mkopo wa kati ya Sh20,000 hadi Sh1 milioni huku wakitozwa riba ya asilimia saba.

Muda wa kulipa mkopo huo ni miezi sita ila wanaokopa wana nafasi ya kuanza kulipa pole pole au hata mara moja.

“Tumewaongezea Sh10 bilioni za kibiashara. Makundi yatakuwa yakipata kati ya Sh20,000 na Sh1 milioni ila kabla upate hiyo milioni, lazima ulipe hela ambazo ulikuwa umekopa,” akaongeza Rais.

Kulingana na takwimu zilizotolewa na Waziri Simon Chelugui mnamo Julai 16, serikali ilikuwa imetoa Sh33 bilioni kama mikopo kwa watu binafsi.

Kati ya pesa hizo, Sh22 milioni zilikuwa zimerejeshwa huku Sh1.6 milioni zikielekezwa kwenye akiba ya waliokuwa wamekopa na kulipa mikopo yao.

Jijini Nakuru, zaidi ya asilimia 77 ya watu 878,000 ambao walikopa pesa za hasla wamelipa huku asilimia 23 wakikosa kutimiza wajibu huo. Kaunti hiyo ilipokezwa Sh2 bilioni za pesa za hazina hiyo.