HabariNews

Azimio na Kenya Kwanza Zaafikiana Masuala 5 Makuu ya Kujadiliana kwenye Mazungumzo

Kamati ya kitaifa ya mazungumzo ya maridhiano kati ya Serikali na Upinzani hatimaye imetia sahihi mfumo maalum utakaowaongoza kwenye mazungumzo hayo.

Viongozi wa Kamati za pande mbili hizo wakiongozwa na Kalonzo Musyoka wa mrengo wa Azimio na mwenzake wa Kenya Kwanza Kimani Ichungw’ah wamesema sasa wapo tayari kuanza mazungumzo pasi kupoteza muda.

Viongozi hao waliafikiana masuala Matano makuu na kutia sahihi kujadiliwa katika mazungumzo hayo.

Haya hapa masuala yaliyoafikiwa:

  1. Uhakiki wa masuala tata ya Katiba hapa wakinuia kuangazia: Kipengee cha 43 cha katiba kinachoangazia gharama ya maisha nchini, Utekelezaji wa ‘thuluthi mbili ya jinsia’ , masuala ya uongozi na pia usawa wa teuzi serikalini.
  2. Masuala ya Uchaguzi, Kamati hiyo itakagua upya Uchaguzi mkuu wa 2022, Suala la mipaka nchini na pia Kuifanyia mageuzi Tume Huru ya Uchaguzi na mipaka, IEBC.
  3. Suala la Kuwekeza fedha katika Katiba; ikihusu Hazina ya Kitaifa ya ustawishaji Maeneobunge, NGCDF, Hazina ya Afya na pia Hazina ya Utendakazi wa Seneti kwa kaunti.
  4. Kadhalika, Kubuniwa kwa Afisi rasmi ya Kinara wa upinzani na pia kuhalalisha Afisi ya Waziri mwenye mamlaka Makuu.
  5. Suala la kuangazia Miungano na vyama vya Kisiasa, kitengo hiki kikishughulikia hujuma na uingiliaji wa vyama vya kisiasa na kuzuia hilo kufanyika.

Viongozi wa pande zote mbili wamewataka wakenya kuwa na subira mazumgumzo yakiendelea na pia kupuuza matamshi yoyote ya wanasiasa yanayonuia kusambaratisha mazungumzo hayo.

“Tunawataka wakenya kuwapuuzilia mbali waropokaji, kawaida kuna wale watahisi kukosa furaha na amani kwa mazungumzo haya, ni kawaida yao kusema. Tayati tushakubaliana mfumo wa kuufanyia kazi kwenye mazungumzo haya,”

 

Wakati huo huo wamewataka wakenya kuwa na matumaini kuhusu mafanikio ya mazungumzo hayo baina ya pande hizo mbili unaolenga kusuluhisha tofauti zao.

“Kwa kweli tumefanya maendeleo makubwa sana katika hili, wahenga walisema ukiona vyaelea ujue vimeundwa. A lot of work has been done ndio sasa vimeanza kuelea, tunawataka kuwahimiza Wakenya kuendelea kuwa na imani na hii team,” alisema Kalonzo.

Kamati hiyo ina siku 60 kujadili na kutoa ripoti na ama kujumuisha miswada inayoainisha kuanzishwa kushughulikiwa kwa sehemu za sheria kadha wa kadha.

NA MJOMBA RASHID